Thursday 14 August 2014

Hujuma nzito



  • Mashine Elektroniki zatumika kuibia serikali
  • Mwigulu aendesha msako, aagiza uchunguzi
  • Kampuni kubwa zahusishwa, wawili mbaroni

NA MWANDISHI WETU
SERIKALI inahofiwa kupoteza mabilioni ya shilingi kutokana na baadhi ya wafanyabiashara kuanza kufanya hujuma kwa kutumia mashine za kielektroniki (EFD) zinazotumika kukusanya kodi.
Hatua hiyo inatokana na kubainika kuingizwa sokoni kwa mashine zinazotoa risiti feki, ambapo kodi inayokatwa kwa mnunuzi imekuwa haiwasilishwi Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).
Hata hivyo, TRA imekuwa ikiwasilishiwa madai ya kurejeshewa fedha kutokana na matumizi ya mashine hizo na baadhi ya kampuni kubwa nchini.

Hujuma hiyo ilibainika jana, wakati Naibu Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, alipoingia mtaani kushiriki kukamatwa kwa Ofisa Utawala Msaidizi wa Kampuni ya Checknocrats, inayouza mashine za  kielektroniki, Jatin Borhara.
Ofisa huyo alidaiwa kuuza mashine za aina hiyo zinazotoa risiti feki baada ya kampuni yake kuiuzia kampuni ya CI Group mashine ambayo inatoa risiti feki hivyo kuisababishia serikali hasara ya mabilioni kwa kulipa mrejesho wa fedha ambazo hazijakusanywa.
Kutokana na tuhuma hizo, serikali imeiagiza TRA, kuangalia mkataba wa kazi wa kampuni hiyo na zingine zilizipewa dhamana kama hiyo.
Pia alisema tukio hilo ni baya kutokea na kwamba wahusika ni lazima wachukuliwe hatua kali za kisheria kutokana na kuhujumu uchumi na kukwamisha shughuli za maendeleo.
Akizungumza katika Ofisi za Checknocrats zilizoko jengo la Msalaba Mwekundu, makutano ya barabara ya Morogoro na Bibi Titi Mohammed, Dar es Salaam, Mwigulu alisema serikali itahakikisha wahusika wanachuliwa hatua ili iwe fundisho kwa wengine.
Alisema mashine hiyo ambayo ni mali ya kampuni ya Checknocrats ambayo ni wakala wa TRA, imetumika kwa kampuni mbalimbali zikiwemo Vodacom, Tigo, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Kampuni ya Bia ya Serengeti na Benki ya NMB na kuwa serikali imekuwa ikilipa gawio kwa kampuni hizo kwa kodi ambayo haijakusanywa.
Alisema walibaini mashine ambayo ina namba 03TZ540000353 au 04TZ100788 baada ya kampuni hizo kutaka rejesho la gawio la kukusanya kodi.
Mwigulu alisema baada ya kutilia shaka, walianza kufanya uchunguzi na kubaini gawio walilotoa kwa kampuni hizo ni makusanyo hewa ambayo yalipitia kampuni ya CI Group.
Hata hivyo, uongozi wa kampuni ya Checknocrats ulikanusha kuiuzia kampuni hiyo mashine.
Walipoulizwa kama waliuza mashine hiyo, walikanusha na kudai ilikuwa inatumika katika ofisi yao ya Mwanza kwa kufundishia wateja wapya namna ya kutumia. Waliongeza  kuwa mashine hizo zinakuwa hazijaunganishwa na TRA.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa CI Group, Fires Nassoro, ambaye naye anashikiliwa kuhusiana na tukio hilo, alisema mashine hiyo aliuziwa katika ofisi hiyo na kwamba wafanyakazi wake hufika mara kwa mara kwa ajili ya kuifanya matengenezo.
Uongozi wa Checknocrats ulimtaka Nassoro aonyeshe risiti zinazoonyesha kuwa aliuziwa mashine hiyo kwa kuwa kumbukumbu zao zinaonyesha ni miongoni mwa zilizoibwa katika ofisi yao ya Mwanza.
Alisema walitoa matangazo kwenye vyombo vya habari Julai, mwaka huu.
Hata hivyo, Mwigulu alihoji ni kwa nini mashine hiyo ambayo ilianza kutumika tangu mwezi Julai, mwaka jana, tangazo la kupotea litolewe Julai, mwaka huu.
Alisema mwisho wa kurushiana mpira kwa watuhumiwa hao utafikia tamati pindi watakapotakiwa kuonyesha vithibitisho.
“Lazima hatua kali zichukuliwe kwa kampuni zote zilizoaminiwa na serikali na zinafanya hujuma za wazi kwa ajili ya utengenezaji na usambazaji wa mashine. Huu ni uhujumu uchumi na katika hili serikali tutasimama imara,” alisema.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru