Monday, 11 August 2014

Mtikisiko CHADEMANa Chibura Makorongo, Simiyu
John Shibuda (Mb) - Maswa
HATIMAYE mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda (CHADEMA), ametangaza hadharani kujiengua ndani ya chama hicho.
Amesema amechoshwa na matusi, kejeli na kuitwa msaliti na kwamba, katika uchaguzi mkuu ujao atagombea ubunge kupitia chama kingine na sio CHADEMA.
Uamuzi huo wa Shibuda ni mwendelezo wa wimbi la wanachama na viongozi wa CHADEMA kukihama chama hicho kutokana na ukandamizwaji wa demokrasia na ubabe wa baadhi ya viongozi.
Baada ya viongozi wa mikoa na wilaya, wimbi la kukitosa chama hicho sasa limehamia kwa wabunge, ambapo Shibuda ameanza kufungua njia.
Akizungumza jana kwenye mkutano wa Baraza la Wazee la Wilaya ya Maswa, Shibuda alisema amechoka kutukanwa, kuitwa msaliti na mnafiki na kuwa, hawezi kuvumilia vitendo hivyo na sasa imetosha.
Alisema tangu amejiunga na CHADEMA akitokea CCM, amekuwa mnyonge kutokana na kuwa mtu wa kutukanwa na kupewa majina ya karaha kila kukicha huku akinyimwa ushirikiano na viongozi wa juu.
Shibuda, ambaye anaaminika kuwa ni mmoja wa wanasiasa wenye misimamo, alisema hawezi kuendeshwa kama mtoto wala kufuata mkumbo kama viongozi wa chama hicho wanavyotaka.

“Tangu nimejiunga CHADEMA ni matusi na kejeli na sasa imefika mahali hata watoto wadogo ndani ya chama hiki wamediriki kunitukana... nimechoka na siwezi kuvumilia hali hii..nimekuwa mvumilivu kwa muda mrefu.

Natangaza sitagombea ubunge nikiwa CHADEMA na ifahamike kuwa hiki chama sio baba wala mama yangu,” alisema Shibuda.

Kuhusu UKAWA
Akizungumzia kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), kususia vikao vya Bunge Maalumu la Katiba, Shibuda alisema kundi hilo halina maslahi kwa Watanzania.
Alisema idadi kubwa ya Watanzania ni wakulima na wafugaji na kwamba, kitendo cha kushindwa kutetea maslahi yao ni usaliti.
Hata hivyo, alisema licha ya yeye kuwa miongoni mwa waliosusia vikao kutokana na msimamo wa chama chake, hakuna taarifa kuhusiana na kinachoendelea mpaka sasa.
Alisema mambo mengi amekuwa akiyasikia kupitia vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na vikao vya maridhiano baina ya UKAWA na CCM.

“Mimi sio mkokoteni na siwezi kuota kuhusiana na maamuzi ya UKAWA, wanajadiliana na wengine wanapewa taarifa lakini kwa Shibuda ni siri kubwa. Sifahamu ni kwanini nabaguliwa,” alisema.


Atangaza kurudi bungeni
Shibuda alitangaza rasmi jana kuwa, atahudhuria vikao vya bunge hilo vinavyoendelea mjini Dodoma kwa ajili ya kuwakilisha wananchi.
“Sipelekwi pelekwi na siko tayari kupelekwa na chama chochote hapa nchini wala viongozi… nitaenda bungeni wiki hii kuendelea na vikao ili  niwatetee wakulima wangu wa pamba pamoja na wafugaji ambao ni maskini,” alisema Shibuda na kuamsha shangwe kwa wazee hao.

Ashusha tuhuma kwa viongozi
Shibuda alisema viongozi wa CHADEMA ni wababe na wabaguzi katika uendeshaji wa chama hicho, jambo ambalo limekuwa likiwakera wanachama wengi.
Alisema viongozi hao wamekosa hekima na busara na kwamba, wamekuwa wakiwaendesha wabunge kufanya wanayoyataka wao na hawapendi kupingwa wala kushauriwa.

“Viongozi ni wababe hawana hekima na busara,  wanataka kuendesha chama watakavyo kana kwamba, ni mali yao hilo kwangu halipo na siwezi kuvumilia hivyo nimekataa. Waliposikia nimetoka CCM walinifuata nijiunge na CHADEMA hivyo, hawawezi kuniendesha watakavyo,” alisema Shibuda.


Atangaza vita na Lissu
Huku akionyesha hasira, Shibuda alisema anachukizwa na Mwanasheria wa CHADEMA, Tundu Lissu, kwa kumwandama bila ya sababu za msingi na kumuonya kuacha mara moja.
Alisema Lissu, ambaye pia ni mbunge wa Singida Magharibi, amekuwa akimfuata fuata na sasa amemua kujibu mapigo kwani amemvumilia kwa kiwango kikubwa.
“Lissu amenishtumu mengi nimemsikiliza na kuvumilia vya kutosha..sasa nikirudi Dar es Salaam tutaonana ... siwezi kutukanwa na mtoto mdogo kama Lissu,” alisema.
Baadhi ya wazee waliohudhulia mkutano huo, walitangaza kumuunga mkono Shibuda kwa uamuzi wake wa kuachana na CHADEMA.
Pia wamemtaka kurejea bungeni kutetea maslahi ya wakulima na wafugaji na kuwa, wataendelea kumuunga mkono katika maamuzi atakayochukua.
Hata hivyo, Shibuda alisema kuwa bado hajaamua atajiunga na chama gani cha siasa huku habari za kuaminika zikisema kuwa, atakwenda chama cha ACT Tanzania.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru