Tuesday, 26 August 2014

TPC yaboresha huduma ya kutuma fedha kwa mitandao

NA WILLIAM SHECHAMBO
SHIRIKA la Posta Tanzania (TPC), limesema liko mbioni kuboresha zaidi huduma zake ikiwemo ya kutuma fedha kwa mitandao ya simu, hatua ambayo itawezesha wananchi kutumia huduma za shirika hilo zitakazokuwa na ubora na unafuu kwa manufaa ya umma.

 
Pia limesema huduma za posta ni muhimu kwa maendeleo ya nchi yoyote duniani licha ya uwepo wa tekinolojia mbalimbali hususan barua pepe na simu za viganjani ambapo hata nchi zilizoendelea bado zinaendelea kutumia mawasiliano ya posta.

Hayo yalisemwa mkoani Dar es Salaam jana, na Meneja Masoko wa shirika hilo David George, alipokuwa akizungumza na gazeti hili juu ya maboresho ya huduma zao kwa kipindi kijacho.

Alibainisha kuwa kipindi kifupi kuanzia sasa wataweka bayana mtandao wa simu nchini ambao utashirikiana na shirika la posta kuongeza ufanisi kwenye huduma yao ya kutuma pesa inayolikana kama 'Postal cash'.

Alisema changamoto kubwa kwenye kazi zao inasababishwa na maendeleo ya sayansi na teknolojia, ambapo Wananchi wamekuwa wakizipuuzia huduma za shirika la posta na kukimbilia njia za kisasa za mawasiliano, hali inayoleta maafa kwa maendeleo ya taifa.

Hivyo ili kwenda sambamba na changamoto hiyo kwa kumridhisha mteja na kuleta ushindani sokoni, alisema walianzisha huduma zingine mbalimbali ikiwemo ya usafirishafi mizigo na vifurushi, utumaji wa pesa na huduma za uwakala ambazo zote zinatumia teknolojia ya haraka na ufanisi.

Alisema kati ya maafa yanayoonekana katika taifa kutokana na watu kutotumia huduma za posta ni ukosefu wa uelewa wa jinsi ya kuandika barua za kiofisikwa idadi kubwa ya watu.

Meneja huyo alisema tatizo hilo ni kubwa licha ya baadhi ya watu kulipa uzito mdogo, kwasababu wasomi wengi hukosa ajira kutokana na kushindwa kukidhi vigezo hasa vya uandishi wa barua za kikazi ambazo hutumika kuomba kazi kwenye taasisi mbalimbali.

Hata hivyo alisema kazi kubwa ilioko kwa shirika ni kusambaza uelewa kwa mwananchi mmoja mmoja, jukumu wanaloendelea kulitekeleza kupitia njia mbalimbali ikiwemo vyombo vya habari kwasababu kampuni na mashirika tayari yana uelewa huo na ni wateja wakubwa wa TPC.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru