Wednesday 6 August 2014

Kibano bungeni


  • Posho sasa kudhibitiwa, Kiti chapewa rungu
  • Kanuni kali kuwabana wajumbe watoro
  • Vinara wa zomea zomea, matusi kukiona

WAJUMBE wa Bunge Maalumu la Katiba, wamependekeza kuwepo kwa kanuni kali za kuwadhibiti wanaozomea na kutoa lugha chafu ili kurejesha heshima ya bunge hilo.
Pia wamependekeza wajumbe wote wanaotoroka kuhudhuria vikao vya Bunge, kutolipwa posho za vikao pamoja na kumpa rungu mwenyekiti la kuwaadhibu wote watakaokwenda kinyume.
Mapendekezo ya mabadiliko ya kanuni hizo, yanatokana na kilio cha wananchi wengi baada ya wajumbe wa bunge hilo kufanya vitendo vya kitoto na visivyoendana na hadhi waliyonayo.

Tangu kuanza kwa bunge hilo Februari, mwaka huu, vitendo vya utovu wa nidhamu, ikiwemo matusi na lugha za kejeli, vimekuwa kitu cha kawaida miongoni mwa wajumbe wa bunge hilo, ambalo limepewa jukumu zito la kuwapatia Watanzania Katiba Mpya.
Akiwasilisha mapendekezo ya kanuni hizo bungeni jana, Mwenyekiti wa Kamati ya Kanuni, Pandu Ameir Kificho, alisema hatua hiyo imelenga kujenga na kuimarisha nidhamu ndani ya bunge.
Alisema mjumbe aliyepewa adhabu kwa mujibu wa kanuni, hatalipwa posho ya vikao ama kujikimu kwa muda wote atakaokuwa akitumikia adhabu.
Hata hivyo, alisema mjumbe ambaye atakuwa amepewa adhabu na tayari amechukua posho, hatalipwa katika vikao vinavyofuata na utaratibu husika utatumika kufidia fedha hizo.
“Mjumbe aliyepewa adhabu kwa mujibu wa kanuni, hatalipwa posho yoyote ya vikao au ya kujikimu kwa kipindi chote, na iwapo posho ilishatolewa, basi itakatwa kutoka katika malipo mengine ya mjumbe husika,” alisema Kificho.
Aidha alisema mapendekezo hayo yatakapopitishwa, kila mjumbe atapaswa kutia saini karatasi ya mahudhurio iliyoandaliwa na kwamba baadaye itawasilishwa kwa Katibu wa Bunge Maalumu.
Kanuni nyingine inayopendekezwa kufanyiwa marekebisho ni ya 36, ambayo inahusu upigaji wa kura wa ibara za Rasimu ya Katiba.
Kwa mujibu wa Kificho, bila kuathiri masharti ya Sheria na Kanuni, ibara za Sura za Rasimu ya Katiba zilizoandikwa upya, zitapigiwa kura katika muda wa siku saba.
Alisema kanuni zingine zilizopendekezwa kufanyiwa mabadiliko ni pamoja na  namba 14, 15, 32, 32b, 33,35,46,47,54,60,62 na 65.
Alisema kamati yake imeshamaliza kazi ya kujadili kanuni hizo kwa mujibu wa maelekezo ya Mwenyekiti wa Bunge.
Wakichangia mapendekezo hayo, wajumbe waliomba kuwepo kwa kanuni kali zitakazoweza kuwabana wajumbe wa Tume ya Marekebisho ya Katiba kuendelea kujadili na kutoa kauli dhidi ya Bunge.
Zainab Gama, alisema ni vyema kukawa na kanuni maalumu ambazo zitamtaka mjumbe yeyote ambaye hajahudhuria kikao kwa muda wa siku 15, afutwe nafasi hiyo.
Alisema kugomea vikao hivyo vya Bunge ni kutumia vibaya nafasi ya uwakilishi katika bunge hilo maalumu.
Kwa upande wake, Dk Ave-Maria Semakafu, alisema ni muhimu kwa bunge hilo kuhakikisha kuwa masuala ya elimu, afya na usawa wa kijinsia vinapata nafasi katika majadiliano ya rasimu hiyo.
Alisema masuala ya muundo wa uongozi si kipaumbele cha wananchi kwani nia ya wananchi ni kupata katiba inayowagusa wananchi katika mambo yao.
SITTA ALALAMA

Mwenyekiti wa Bunge hilo, Samuel Sitta, amelalamikia baadhi ya vyombo vya habari ambavyo vimekuwa vikitumika kuendesha midahalo inayowadhalilisha wajumbe wa bunge hilo.
Alisema vyombo hivyo vimekuwa vikirusha vipindi hivyo moja kwa moja, ambapo washiriki wamekuwa wakiegemea upande mmoja huku wengine wakitoa lugha chafu zenye kuudhi pamoja na kuwazomea wengine wanaoonekana kuwa upande tofauti.
ìInashangaza kuona watu hawa wanapewa nafasi na ni wale wale kila siku. Hebu Mama Mukangara (Dk. Fenella-Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo), angalia kuna nini huko, lakini pia nadhani serikali inasikia hili,” alisema.
Hivi karibuni, vituo kadhaa vya luninga vimekuwa vikirusha midahalo kuzungumzia Katiba Mpya, ambapo baadhi ya washiriki wamekuwa wakitumia lugha za kuudhi.
Mjumbe Thomas Mgoyi, alisema tume imeshafanya kazi yake na imemaliza, hivyo inabidi waachane na kulishambulia Bunge  Maalumu la Katiba.
"Watuache tufanye kazi za wananchi kuliko kutusema na kututukana maana tutashindwa kuvumilia,î alieleza.
MMANDA AZUNGUMIA RASIMU
Mmoja wa wajumbe wa Kamati ya Kanuni, Evod Mmanda, alisema bunge hilo lina uwezo wa kujadili Rasimu ya Katiba iliyowasilishwa na Tume ya Jaji Warioba.
Alisema bunge hilo lina nguvu na mamlaka ya kujadili na hata kuboresha kilichowasilishwa kabla ya kwenda kupigiwa kura na wananchi.
Hata hivyo, alisema hakuna kanuni za kuwabana wanaoandaa midahalo nje ya bunge kwa kuwa, kanuni zinahusu kungíata wajumbe ndani ya bunge.
Pia alisema kanuni wala sheria hazisemi iwapo wajumbe wa kundi la 201, wanaweza kuadhibiwa iwapo watatoka ndani ya bunge kwa kuwa sheria haisemi kama wanaweza kufukuzwa.
Mmanda alisema sheria ipo wazi kuwa, iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, ilishamaliza kazi yake na waliokuwa wajumbe wake wanazungumza kwa utashi wao.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru