NA SHAABAN MDOE, ARUSHA
KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas
amemzima mbunge wa Arusha, Godbless Lema kwa kumweleza kuwa jeshi hilo haliwajibiki
kutoa taarifa za uhalifu kwa Waziri Kivuli wa Wizara ya Mambo ya Ndani.
Kauli ya Kamanda Sabas imetokana na Lema kudai kuwa jeshi
hilo haliwasilishi kwake taarifa za matukio ya kihalifu yanayotokea Arusha na kwamba,
hiyo inaonyesha ni dharau.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda Sabas
alisema polisi hawawajibiki kutoa taarifa za kihalifu kwa Lema na kwamba,
taarifa za kihalifu zinatolewa kwa Waziri kamili wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya
Nchi, ambayo inaongozwa na Mathias Chikawe.
“Hatushughuliki na Waziri Kivuli wakati mwenye dhamana kisheria yupo, hayo mambo ya vivuli ni huko huko bungeni na sio kwetu. Hatuna utaratibu wa kutoa taarifa zetu kwa waziri kivuli wala mbunge,” alisema Kamanda Sabas.
Hivi karibuni, akihutubia mkutano wa hadhara katika
Viwanja vya Samunge, Lema alidai hashirikishwi kwenye uamuzi wa kuanzisha mfuko
kuisaidia polisi kupambana na uhalifu jijini hapa.
Kwa mujibu wa Sabas, alisema si mara ya kwanza kwa Lema
kulitupia lawama jeshi hilo kwa lengo la kulichafua mbele ya jamii ili apate
umaarufu.
Alisema baada ya matukio ya kulipuliwa kwa mabomu
katika maeneo mbalimbali ya jiji la Arusha, likiwemo la mkutano wa CHADEMA uliofanyika
uwanja wa Soweto, Lema alilituhumu jeshi hilo kuhusika na mlipuko huo.
Pia alisema Lema alishawahi kuharibu uhusiano
uliokuwepo baina yake na jeshi hilo na kwamba, siku zote hakubali kazi
inayofanywa na jeshi hilo.
Alisema Lema anatakiwa kujiuliza kwanini kama mwakilishi
wa wananchi hajashirikishwa katika kuanzisha mfuko maalumu wa fedha kwa ajili
ya ulinzi wa raia na mali zao na sio kulilaumu jeshi la polisi kuwa halijamshirikisha
katika mpango huo.
Kamanda Sabas alisema uamuzi wa kuanzishwa kwa mfuko
huo hauakutolewa na jeshi la polisi na kwamba, ni wananchi wenyewe
waliohudhuria katika mkutano wa polisi na wadau wa usalama.
Alisema mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa bwalo
la polisi, Agosti 14, mwaka huu.
RPC Liberatus Sabas - Arusha “Ni vyema Lema akafahamu kuwa sisi sio tuliomba kuchangiwa hizo fedha bali wananchi ndiyo waliamua kuwepo kwa mfuko huo, hivyo ni vyema akawaulize anaodai kuwaongoza," alisema.
Hata hivyo, alimtaka Lema kuunga mkono juhudi hizo
badala ya kuzipinga kwa maslahi yake binafsi.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru