Thursday, 7 August 2014

Ofisa Usalama kizimbani kwa mauaji ya bosi wake


NA FURAHA OMARY
OFISA Usalama wa Taifa, Mohammed Kazembe, anayetuhumiwa kumuua bosi wake, amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kwa shitaka la mauaji, akiwa hoi hajiwezi.
Kazembe (33), alifikishwa mahakamani hapo jana asubuhi, akiwa amebebwa na watu wawili huku mguu wake wa kushoto ukiwa umefungwa bandeji kutoka kwenye kisigino hadi ugokoni na mkononi alikuwa na njia ya kuwekea dripu ya maji.
Mshitakiwa huyo, mkazi wa Mwananyamala, ambaye hakuwa na uwezo wowote wa kutembea, alifikishwa mahakamani hapo mbele ya Hakimu Mkazi, Frank Moshi, akiwa na washitakiwa wenzake watatu.
Washitakiwa hao ni mfanyabiashara Lucy Mwafongo (43), mkazi wa Vingunguti, madereva Omary Liwanga au maarufu kwa jina la Sheikh Ponda (26), mkazi wa Mbagala Mwandege na Kelvin Lilai (28), mkazi wa Mbagala Kiburugwa.
Kazembe anayetetewa na Wakili Deiniol Msemwa na wenzake, walisomewa shitaka hilo na Wakili wa Serikali, Celina Kapange.
Celina alidai Aprili 29, mwaka huu, maeneo ya Njia Panda ya Uwanja wa Ndege, wilayani Ilala, mkoani Dar es Salaam, kwa makusudi, walimuua Silvanus Mzeru, ambaye alikuwa Ofisa Usalama wa Taifa.
Washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo. Celina alidai upelelezi haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Hata hivyo, kabla ya kuahirishwa kwa kesi hiyo, Wakili wa Kazembe, Msemwa, alidai mteja wake ni mgonjwa na ana majeraha makubwa, hivyo aliomba upande wa Jamhuri kukamilisha upelelezi mapema ili shauri liende Mahakama Kuu ya Tanzania.
Pia aliomba mshitakiwa kutokana na hali yake, awekewe mazingira mazuri.
Alidai mshitakiwa huyo kabla ya kuingizwa katika chumba cha mahakama, aliwekwa katika korido ambapo kila mtu alikuwa akiruka katika mguu wake.
Hakimu Moshi aliusisitiza upande wa Jamhuri kuhakikisha kuwa mshitakiwa analetwa katika mazingira salama na maradhi yanayomkabili yatashughulikiwa na Jeshi la Magereza.
Kesi hiyo iliahirishwa hadi Agosti 20, mwaka huu.
Baada ya kumaliza kusomewa shitaka hilo, Kazembe, Lilai, dereva Revocatus Rugarabamu (23), mkazi wa Tabata Segerea na Lucy, walipanda tena kizimbani mbele ya Hakimu Frank, wakikabiliwa na kesi nyingine ya mauaji.
Wakili Celina alidai Julai 25, mwaka huu, maeneo ya barabara ya Haile Sellaise, Oysterbay, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, walimuua Frank Silayo.
Washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote na walirudishwa rumande hadi Agosti 20, mwaka huu, kesi itakapotajwa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru