NA SHAABAN MDOE,ARUSHA
ZAIDI ya wanafunzi 350 wa Chuo Kikuu Cha Mtakatifu Joseph, tawi la Arusha, wamegoma kuingia madarasani kwa madai ya kufundishwa kwa mitalaa kutoka nchini India.
Mbali na hilo, wanafunzi hao ambao wanasomea ualimu, wanadai kufundishwa na walimu wenye fani ya uhandisi na kwamba huimbishwa nyimbo za darasa la kwanza, pili na tatu.
Kiongozi wa Chuo hicho, Bwigane Mwaipaja, alisema tokea mwanzo wa muhula wa masomo, walibaini kuwepo kwa mitaala tofauti katika chuo hicho.
Alisema chuo hicho kinatofautiana na vyuo vingine kutokana na kufundishwa kwa kutumia mitaala kutoka nchini India, ambayo haiendani na mitaala ya Tanzania.
Mwaipaja alisema wanafunzi hao hawafundishwi masomo ya vitendo, badala yake wanafundishwa kuimba nyimbo za darasa la kwanza, pili na tatu.
Alisema mapungufu mengine katika chuo hicho ni kwamba wanafunzi wanafundishwa na walimu wenye fani ya uhandisi, ambao hawana taaluma ya ualimu.
Mwaipaja alisema baada ya wanafunzi kubaini kasoro hizo, waliwasilisha malalamiko yao katika uongozi wa chuo hicho, ambao uliahidi kulipatia ufumbuzi muhula wa pili wa masomo utakapoanza, lakini halikupatiwa ufumbuzi.
Alisema walizungumza na walimu wao ambao walidai hawana taaluma ya kufundisha masomo ya ualimu.
Mwanafunzi Rehema Swai, alisema mtaala huo wa India hauna muhuri kutoka TCU na kwamba wanaiomba serikali itoe tamko iwapo mtaala huo unafaa kufundishwa nchini.
Kwa mujibu wa Rehema, hulazimishwa kutafuta manyoya ya kuku au ndege na kuyagandisha kwa gundi katika madaftari ya somo la mazoezi, tofauti na vyuo vingine.
Alisema elimu wanayopatiwa chuoni hapo ni sawa na kupoteza muda na fedha na kwamba hawawezi kuitumia sehemu yoyote.
Mwalimu msaidizi wa chuo hicho, Josephat Tambu, alikiri kuwepo kwa malalamiko ya wanafunzi hao ambapo alisema suala hilo linahitaji muda kutatuliwa.
Alisema chuo hicho hakina uhaba wa walimu na kwamba tatizo la kuwepo kwa walimu wasio na uwezo litapatiwa ufumbuzi baada ya muhula wa masomo kumalizika.
Thursday, 14 August 2014
Wanafunzi St.Joseph wagoma kuingia darasani
01:17
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru