RAIS wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi, amesema serikali haijawahi kufuta Azimio la Arusha kama inavyodaiwa na baadhi ya wananchi.
Hata hivyo amesema kilichofanyika ni ilizimua azimio hilo kuwapatia viongozi wa kati uwezo wa kumudu makali ya maisha.
Mwinyi alisema hayo jana jijini Dar es Salaam katika semina ya siku moja ya maandalizi ya sheria ya kudhibiti mgongano wa maslai miongoni mwa viongozi na watumishi wa umma iliyoandaliwa na Sekretarieti ya Maadili ya viongozi.
“Serikali haikufuta Azimio la Arusha. Ililizimua azimio hilo kuwapatia viongozi wa kati kumudu makali ya maisha. Lakini baadhi ya viongozi wamekuwa wakitumia vibaya nafasi hiyo kuvunja sheria ya maadili ya viongozi,” alisema.
Kutokana na tabia hiyo, alisema: “Baadhi ya watu wamekuwa wakitumia vibaya nafasi hiyo kuvunja maadili ya viongozi wa umma kwa kutumia rasilimali za umma kujinufaisha. Hii imewafanya wananchi kutokuwa na imani na viongozi wao.”
MASLAHI BINAFSI TATIZO
Kwa mujibu wa Mwinyi, mgongano wa maslahi ini tatizo kubwa nchini linalotakiwa kuangaliwa kwa umakini, vinginevyo baadhi ya viongozi wataendelea kujinufaisha kwa kutumia madaraka na nafasi zao.
Alisema vita dhidi ya mgongano wa maslahi iliasisiwa na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere, baada ya kupata uhuru, ambapo kulikuwa na miiko ya uongozi iliyofafanuliwa kwenye Azimio la Arusha la mwaka 1967.
“Moja ya miiko ile ilikuwa viongozi wa umma kutokuwa na mshahara zaidi ya mmoja na pia kutotakiwa kuwa na nyumba ya kupangisha, lengo kuu likiwa kuhakikisha viongozi wanautumikia umma ipasavyo,” alisema.
Alisema serikali ilizima ukali wa Azimio la Arusha ili kuwaruhusu viongozi wadogo wa umma kujitafutia kipato cha ziada ili kumudu gharama za maisha na kupata haki ya kikatiba ya uhuru wa kuwa na mali ya akiba ya kumwokoa wakati wa dharura.
Kiongozi huyo alisema sasa hali ni kinyume na ilivyotarajiwa kwa sababu watu wanatumia vibaya haki ya kikatiba kwa kumiliki mali hata kwa njia zisizo halali.
Alisema tatizo la viongozi waliopewa dhamana kutumia rasilimali za umma kwa ili kujinufaisha binafsi ni kubwa na limezikumba nchi nyingi duniani ila zinatofautiana ukubwa na namna wanavyolitafsiri.
Pia alisema sheria hiyo inawabana baadhi tu ya viongozi wanaotajwa kwenye sheria hiyo na kanuni zake na kuacha huru viongozi wengine wengine na watumishi wa umma kwa ujumla kuhusiana na suala la kujiingiza kwenye mgongano wa maslahi.
“Viongozi na watumishi wa umma wanatakiwa kuweka kipaumbele kwa maslahi ya umma kuliko maslahi binafsi, ikiwemo kutofanya shughuli za kibiashara na taasisi wanazozisimamia,” alisema.
Alishauri utumike mfumo utakaowataka viongozi kuweka mali zao kwenye kampuni ya udhamini na kuiachia kuendesha biashara husika bila mwenye mali kuhusishwa moja kwa moja lengo ni kudhibiti matumizi mabaya madaraka.
Alisema hali ya ukuaji wa uchumi wa nchi haukidhi hali ya vipato na maisha ya wananchi wa kawaida jambo ambalo halitoi picha nzuri wa Tanzania ambayo inarasilimali nyingi.
Alisema hali hiyo imesababisha malalamiko baina ya wananchi kuwa viongozi wao wamekuwa wakitumia vibaya rasilimali za umma na kutumia vibaya madaraka waliyopewa na umma hivyo kupoteza imani waliyonayo kwa serikali.
JAJI KAGANDA ALONGA
Kwa upande wake Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji (mstaafu) Salome Kaganda, alisema lengo na makusudi ya mapendekezo ya sheria hiyo ni kuleta amani na utulivu wa nchi.
Jaji Salome alisema: “Mapendekezo ya sheria hii hayalengi kuwafanya viongozi kuwa maskini, bali kasi yao ya ukwasi iendane na hali halisi ya kipato chao.
“Sheria hii itakapopitishwa na ngazi husika, itapunguza ubinafsi wa viongozi walioko madarakani kujipendelea na maeneo wanayotoka. Lazima kuwepo na hatua ya serikali kurejesha maadili ya viongozi. Kama itazingatiwa na kuheshimiwa, taifa litafikia maendeleo ya haraka yaliyokusudiwa.”
Kutokana na kukithiri kwa tatizo hilo, alisema mgongano wa maslahi bado ni tatizo ambalo linahitaji kutazamwa kwa jicho la pekee kwa maslahi ya umma.
Alisema kutokana na ukubwa wa tatizo hilo, Rais Jakaya Kikwete amekuwa akikemea mara kwa mara mienendo ya matumizi mabaya ya ofisi na madaraka ya umma, ikiwemo mgongano wa maslahi.
Thursday, 21 August 2014
Azimio la Arusha halijafutwa- Mwinyi
02:51
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru