Wednesday, 27 August 2014

Mkapa: Maslahi binafsi yanaathiri uwajibikaji


NA RABIA BAKARI
RAIS Mstaafu Benjamin Mkapa, amesema mgongano wa kimaslahi baina ya viongozi na watumishi wa umma, ni janga ambalo halijapewa uzito wa kutosha katika kulipatia ufumbuzi.
Amesema tatizo hilo limekuwa likizikumba nchi mbalimbali duniani na kwamba viongozi wenye maslahi binafsi ni tatizo katika kuleta usawa na uwajibikaji.


Akizungumzia wakati akifungua warsha ya kujadili Mapendekezo ya Sheria Mgongano wa Kimaslahi miongoni mwa watumishi wa umma mjini Dar es Salaam, jana, alisema tatizo hilo limekuwepo tangu Uhuru.
Alisema tatizo hilo linajidhihirisha kwa namna  ambayo wenye mamlaka au watoa uamuzi wanapokuwa katika maslahi na jambo fulani,  kutumia madaraka yao badala ya kutoa kipaumbele kwa maslahi ya umma.
Katika warsha hiyo iliyoandaliwa na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Rais Mkapa alisema tatizo hilo haliko nchini pekee, bali duniani kote na katika baadhi ya nchi wameweka na sheria ya kuhakikisha mtumishi wa umma haruhusiwi kuwa na biashara bila kibali maalumu.
Mbali na hilo, pia hutakiwa kujiepusha na mazingira yanayoweza kumwingiza kwenye mgongano wa maslahi wakati wote.
“Msukumo huu wa kudhibiti mgongano wa maslahi kwa kuandika sheria rasmi ni mwendelezo tu wa vita hii. Miaka ya 1960 tulikuwa na mifumo ya kudhibiti tatizo hili kwa viongozi wa umma ambayo lilifafanuliwa katika Azimio la Arusha la mwaka 1967.
“Azimio la Arusha lilimzuia kiongozi wa Chama na serikali kutokuwa na hata nyumba ya kupangisha au kuwa na mshahara zaidi ya mmoja. Kwa  bahati mbaya baada ya Azimio la Arusha hakuna mwongozo wala sheria inayosimamia tatizo hili zaidi ya makatazo yanayotajwa kwenye baadhi ya sheria.
“Ni vyema sasa makatazo haya yakaainishwa katika sheria moja ili kuondoa ombwe la kisheria na kuimarisha usimamizi wa suala hili,” alisema.
Aliongeza kuwa wananchi wamekuwa wakilalamikia viongozi kutumia vibaya rasilimali na madaraka waliyopewa na umma, hivyo kupoteza imani waliyo nayo kwa serikali.
Mkapa alisema athari kubwa anayoiona ni mtazamo hasi wa baadhi ya wanajamii kuweka kipaumbele maslahi ya umma, kwamba siku hizi imejengeka katika ubinafsi kuliko kuangalia maslahi ya yenyewe.
Alisema kinachohitajika ni kuelimisha umma ili kubadilisha kwanza mtazamo wa jamii na iwapo itafanikiwa katika hilo, kazi itakuwa rahisi  kujenga uchumi ambao ndani yake kuna ushindani wa haki na usawa.
Alisema Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma ilianza kutumika akiwa madarakani, na wakati huo na hata sasa hajawahi kuona tatizo la sheria hiyo. 
“Kinachosisitizwa hapa ni ukweli na uwazi kwenye kuchuma mali, kinyume na hapo ni ukiukwaji wa sheria. Ni kweli kuwa taasisi hii (Sekretarieti ya Maadili) ilianzishwa kwa lengo la kusimamia na kukuza maadili, hususan mienendo ya viongozi wa umma,“ alisema.
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Mstaafu Joseph Warioba, alisema utungwaji wa sheria hiyo mpya ni mwendelezo wa maoni ya wengi kuhakikisha uwajibikaji na uwazi katika uongozi unazingatiwa.
Pia alisema itasaidia kuipa meno Sekretarieti, ambapo jambo hilo imesisitizwa hata kwenye Rasimu ya Pili ya Katiba ambayo inajadiliwa katika Bunge Maalumu la Katiba. 
Awali, Kamishna wa Maadili, Jaji Mstaafu Salome Kaganda, alisema miongoni mwa madhara ya mgongano wa maslahi ni pamoja na uchumi wa nchi kudidimia, wananchi kukosa haki za msingi, kuathiri maamuzi na michakato ya kidemokrasia na wananchi kupoteza imani na serikali.
Kwa kifupi, yaliyomo ndani ya mapendekezo ya sheria hiyo mpya nchini ni iwapo itapitishwa viongozi wa umma watachagua ama kuwa na baishara au kubaki katika uongozi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru