Kikosi kazi chaanza mafunzo maalumu
NA WAANDISHI WETU
MIKAKATI ya kudhibiti ugonjwa wa Ebola inazidi kushika kasi, ambapo serikali imetoa mafunzo kwa mamia ya watumishi wa afya watakaokwenda kuhudumia abiria wanaoingia na kutoka nje ya nchi.
Pia vifaa ya kudhibiti ugonjwa huo vinatarajiwa kuingia nchini muda wowote, ikiwemo mashine maalumu za kutambua virusi vya Ebola ndani ya mwili, hata kama aliyeambukizwa bado hajaanza kuonyesha dalili.
Kwa upande wa mafunzo, ambayo yameanza kutolewa jana,Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Stephen Kebwe, alisema yameanza kwa kuwahusisha wahudumu kutoka ndani ya wizara pekee .
Alisema kundi la pili ambalo linaingia mafunzo leo ni lile linalohusisha wahudumu wa afya wa kada nyingine pamoja na wadau waliomo katika kikosi kazi cha kudhibiti ugonjwa huo.
“Ijumaa (kesho) mafunzo yatatolewa kwa wahudumu wa afya kutoka mikoa yenye viwanja vya ndege na mipaka. Hawa wanaopata mafunzo watakuwa walimu wa wengine huko waendako kwa sababu serikali haina uwezo wa kumfikia kila mmoja na kumfundisha,” alisema.
Kuhusu vifaa, alisema serikali imeshaviagiza na ndani ya mwezi huu kila kitu kitakuwa kimekamilika, ikiwemo kupita viwanja vya ndege kwa kukaguliwa na mashine maalumu zenye uwezo wa kugundua virusi vya ugonjwa huo.
Kagera yachukua tahadhari
Mkoa wa Kagera ambao wananchi wake wengi wanaingiliana na nchi jirani za Uganda na Rwanda, wametakiwa kuanza kujikinga na ugonjwa huo, ikiwemo kutoa taarifa kwenye vituo vya afya wanapoona mtu mwenye dalili.
Mkuu wa mkoa huo, Kanali Mstaafu Fabiani Massawe, alisema jana kuwa wamechukua tahadhari kutokana na mwingiliano mkubwa wa shughuli za kijamii katika mipaka na nchi jirani.
Alisema iwapo nchi jirani zitapata ugonjwa huo, Kagera haiwezi kuwa salama, hivyo ni lazima hatua zichukuliwe mapema.
Aliwataka wananchi kila mmoja kuwa mlinzi wa mwenzake na kutoa taarifa pindi wanapoona wana dalili za ugonjwa usioeleweka.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru