Wednesday, 13 August 2014

Swala yaingia soko la hisa


NA MWANDISHI WETU
KAMPUNI ya mafuta na gesi ya Swala, imeingizwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), baada ya kukidhi vigezo vya masoko ya mtaji .
Swala imekuwa kampuni ya kwanza ya mafuta na gesi kutoka ukanda wa Afrika Mashariki kuingia kwenye soko la hisa. 
Hafla ya kuingizwa DSE, ilifanyika juzi  mjini Dar es Salaam, ambapo Rais Mstaafu wa awamu ya pili, Ali Hassan Mwinyi,  ambaye alikuwa mgeni wa heshima, alipiga kengele kuashiria uzinduzi wa kampuni hiyo kuingia DSE. 
Akizungumza baada ya uzinduzi huo, Mwinyi alisema kampuni hiyo ya mafuta na gesi itakuwa chachu kwa Watanzania wengine kujitokeza na kujenga utamaduni wa kuwekeza.
Alisema watu wakiwekeza watasaidia ukuzaji wa uchumi na wao kujiamini kwenye soko la mitaji nchini.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa DSE, Moremi Marwa, alisema kampuni hiyo inakuwa ya 20 katika orodha ya soko la hisa na ya pili chini ya mpango wa kampuni zinazokuwa sokoni (EGM).
Alisema Oktoba, mwaka jana, walizindua mpango huo wa EGM wakiwa na lengo la kuziwezesha kampuni ndogo na zile za kati kuingia katika soko la mitaji.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru