Tuesday 26 August 2014

Dk. Sheni apangua mawaziri, Ma-RC



Na mwandishi wetu, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Sheni, amefanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri pamoja na wakuu wa mikoa na wilaya.
Mabadiliko hayo yanalenga kuendelea kuimarisha utendaji wa shughuli za serikali na tayari jana, amewaapisha wateule wote katika Viwanja vya Ikulu mjini Zanzibar.
Walioapishwa jana ni Dk. Sira Ubwa Mamboya, ambaye anakuwa Waziri wa Kilimo na Maliasili. Aliyekuwa Waziri wa Afya, Juma Duni Haji, amebadilishwa kwenda kuongoza Wizara ya Miundombinu na Mawasiliano na nafasi yake kujazwa na Rashid Seif Suleiman.
Wengine walioapishwa ni Mahmoud Thabi Kombo, ambaye anakuwa Naibu Waziri wa Afya. Katika mabadiliko hayo pia wamo wakuu wa mikoa ambapo, Meja Mstaafu Juma Kassim Tindwa anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Omar Khamis Othman anakuwa Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, Mwanajuma Majid Abdulla kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Ayub Mohamed Mahmoud kuwa Mkuu wa Wilaya ya Magharibi pamoja na Hanuna Masoud Ibrahim, ambaye anakuwa Mkuu wa Wilaya ya Chake Chake Pemba.
Hafla hiyo, ilifanyika Ikulu mjini Zanzibar na kuhudhuriwa na viongozi mbali mbali akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Abdalla Mwinyi Khamis, Mufti Mkuu wa Zanzibar, Sheikh Saleh Omar Kabih, Kadhi Mkuu wa Zanzibar Sheikh Khamis Haji na Meya wa Manispaa ya Mji wa Zanzibar Khatib Abrahman Khatib.
Kabla ya uteuzi huo, Dk. Sira alikuwa Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, ambaye hivi sasa anajaza nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Waziri wa wizara hiyo, Suleiman Othman Nyanga.
Meja Mstaafu Kassim Tindwa alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, ambaye kwa hivi sasa anajaza nafasi iliyowachwa wazi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Pembe, Mwajuma Majid Abdulla alikuwa Mkuu wa Wilaya ya ChakeChake Pemba, ambaye kwa hivi sasa amepanda kuziba nafasi ya Meja Mstaafu Tindwa.
Omar Khamis Othman alikuwa Mkuu wa Wizaya ya Wete, ambaye hivi sasa najaza nafasi iliyowachwa wazi na aliyekuwa Mkuu wa Mkoa huo, Dadi Faki Dadi, Ayoub Mohamed Mahmoud alikuwa Ofisa Tawala Mkoa wa Mjini Magharibi, ambaye hivi sasa anajaza nafasi iliyowachwa na aliyekuwa Mkuu wa Wizaya hiyo, Hassan Mussa Takrima.
Kwa upande wake, Hanuna Masoud Ibrahim alikuwa Ofisa Tawala Mkoa wa Kusini Pemba ambaye hivi sasa anajaza nafasi ya aliyekuwa Mkuu wa wizaya hiyo, Mwanajuma Majid Abdulla.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru