Thursday, 7 August 2014

UKAWA yapasuka



  • Wabunge CHADEMA wahudhuria bungeni
  • Hotuba ya Sitta gumzo, zaidi watarajiwa
  • Kamati zaanza kujadili Sura ya 12 ya Rasimu 

NA WAANDISHI WETU, DODOMA
MPASUKO miongoni mwa wajumbe wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), umezidi kushika kasi huku baadhi wakiamua kuasi na kuhudhuria vikao vya Bunge Maalumu la Katiba.
Kundi la UKAWA, ambalo limesusia kushiriki vikao vya bunge hilo, linaundwa na wajumbe kutoka vyama vya CHADEMA, NCCR-Mageuzi na CUF, ambapo jitihada za makundi mbalimbali nchini, wakiwemo viongozi wa dini kuwataka kurejea bungeni na kushindana kwa hoja, zimeonekana kugonga mwamba.
WAJUMBE  wa Bunge Maalumu la Katika ambao pia ni Wabunge wa Bunge la Tanzania, Letcia Nyerere (Viti Maalumu -CHADEMA) na Mbunge wa Korogwe Vijijini, Stephen Ngonyani 'Profesa Majimarefu', wakiwasili Viwanja vya Bunge, Dodoma, jana.
Hata hivyo, kuna madai ambayo mpaka sasa yameshindwa kuthibitishwa ama kukanushwa na kundi hilo kuwa, wamekuwa wakiwezeshwa na taasisi fulani za nje kwa lengo la kukwamisha mchakato wa kuwapatia Watanzania Katiba Mpya.
Imebainika kuwa baadhi ya wajumbe wanaounda kundi hilo, wameanza kujisajili mmoja baada ya mwingine kurejea bungeni, huku usiri mkubwa ukitawala. Hatua hiyo imetokana na tishio lililowekwa na viongozi wa UKAWA kuwa wajumbe watakaosaliti watakiona cha moto.
Miongoni wa wajumbe hao ni Leticia Nyerere (Viti Maalumu-CHADEMA), ambaye jana alifika ofisi za Bunge mjini hapa kujisajili tayari kwa kushiriki vikao hivyo.
Mapema wiki hii, Leticia alikaririwa akisema kuwa, anajali maslahi ya taifa kwanza na kwamba, kushiriki ama kutoshiriki kwenye bunge hilo kutategemea maamuzi ya viongozi wake.
Jana, mbunge huyo alionekana katika viunga vya viwanja vya Bunge akienda kujisajili, lakini aligoma kuzungumza baada ya kutakiwa kueleza sababu za kupuuza agizo la viongozi wake wa UKAWA.
Jitihada za waandishi wa habari kumbana mbunge huyo hazikuzaa matunda, kutokana na muda wote kuzungumza na simu yake ya mkononi huku akitokomea.
Mbali na Leticia, mwingine ambaye anadaiwa kuwa tayari amejisajili kuhudhuria vikao hivyo ni Mbunge wa Maswa Magharibi (CHADEMA), John  Shibuda.
Habari zaidi zimedai kuwa, Shibuda ambaye siku zote amekuwa mstari wa mbele kutetea maslahi ya taifa, alijisajili juzi asubuhi licha ya kuwa hajaonekana kwenye vikao vinavyoendelea.
Hata hivyo, jitihada za kumpata Shibuda kuzungumzia suala hilo hazikuweza kufanikiwa kwani hata alipotafutwa kupitia simu yake ya kiganjani, ilikuwa ikiita bila kupokewa kabla ya muda mfupi kuzimwa kabisa.

Kamati zaanza kazi
Wajumbe wa bunge hilo jana walianza vikao vya kamati kujadili sura 12 za Rasimu ya Mabadiliko ya Katiba huku hali ya utulivu na maelewano ikitawala.
Baadhi ya wajumbe wamesema hali hiyo inaongeza matumaini kuwa, kazi ya kuandaa Katiba Mpya ya Watanzania iliyo bora itafanyika kwa umakini mkubwa.
Abdalah Bulembo, alisema vikao vimeanza katika hali ya utulivu na Watanzania wategemee Katiba Mpya bora na yenye kujali maslahi ya wanyonge.
Alisema wajumbe wamekuwa na ari kubwa na hotuba ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta aliyoitoa juzi wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, imewaweka sawa kimawazo na kuwafumbua macho walio wengi, hasa kutokana na kauli za uchochezi na ghiliba zinazofanywa na UKAWA.
‘’Katiba bora na yenye kujali maslahi ya wanyonge itapatikana bila wachache wenye malengo na mitizamo binafsi. Hotuba ya Sitta imezidi kuwafumbua watu macho na sasa utulivu na umakini kwa wajumbe wote ni mkubwa,” alisema.
Kuhusu upigaji kura ili kupata theluthi mbili kila upande wa Jamhuri katika maamuzi ya kupitisha Sura za Rasimu, Bulembo alisema hilo si tatizo na kwamba theluthi mbili itapatikana.
Hata hivyo, alisema iwapo hilo litashindikana kutoka kila upande, wajumbe wamekamilisha kazi ya kufanya marekebisho na wananchi ndio watakuwa waamuzi wa mwisho.
‘’Tusitumie unajimu katika upatikanaji wa hizo theluthi mbili, wacha tumalize kazi tuliyotumwa na kama kuna lolote, wananchi wapo wataamua nini cha kufanya wakati wa kupiga kura,” alisema na kuongeza: 
“Watanzania wengi wanatambua nani anafanya nini katika kulinda na kudumisha taifa. Hawa wenzetu wamekuwa na ugomvi na CCM, lakini hii Katiba si ya CCM, ni ya wananchi, hivyo wanapaswa kuweka pembeni tofauti hiyo na kuweka mbele maslahi ya wananchi.’’
Naye Mansour Sharif, alisema upigaji wa kura si suluhisho katika kupata katiba iliyo bora kwani, bado wananchi wana nafasi katika kuangalia utungaji huo.
Alisema siku 60 walizopewa na Rais ni siku muhimu katika kufanya kazi hiyo ya wananchi na kamwe wananchi wasipotoshwe kuwa kazi hiyo haitawezekana.
Stephen Ngonyani, alisema kuna umuhimu wa kuanzisha utaratibu wa kutoa Katiba kwa wananchi mara inapopatikana ili waweze kuisoma na kuelewa kabla ya kufanyiwa marekebisho.
Alisema kwa sasa hali hiyo imejitokeza kwa wananchi walio wengi kutoijua Katiba Katiba ya sasa kikamilifu hivyo kuwa rahisi kupotoshwa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru