Monday 1 July 2013

Dar yazizima ujio wa Obama


NA FURAHA OMARY
KUWASILI kwa Rais Barack Obama jijini Dar es Salaam, jana, kulilifanya eneo lote la katikati ya jiji kuzizima, huku mfumo wa maisha, uendeshaji wa shughuli za ofisi na biashara kuchukua sura mpya ambayo haijawahi kutokea.
Ikiwa ni muda mfupi kabla hajapita katika eneo hilo kuelekea Ikulu, wafanyakazi katika majengo ya maghorofa walipigwa marufuku kukaa upenuni mwa majengo au sehemu ya juu ya majengo hayo, hali kadhalika kuchungulia madirishani.
Sambamba na hayo, barabara ya Sokoine ambayo ndiyo aliyopita Rais Obama, hasa kuanzia eneo la Kituo Kikuu cha Polisi hadi Ikulu, umati mkubwa wa wananchi ulifurika kushuhudia ujio huo.
Hata hivyo, wananchi hao waliamliwa na askari polisi waliokuwa wakilinda usalama kusimama upande mmoja ulikopakana na bahari ya Hindi, na kwamba ilikuwa marufuku kwa mtu kusimama upande wa pili.
Maelekezo hayo yalitolewa na askari wa usalama barabarani waliokuwa wakizunguka kutoka eneo moja hadi jingine kwa kutumia pikipiki aina ya Bajaj.
Wakati askari hao wa usalama barabarani wakiendelea na shughuli zao, helikopta ya polisi ilikuwa ikifanya doria, huku trafiki wengine wakitoa maelekezo kwa kutumia vipaza sauti kwa staili ya kuamuru watu watekeleze lile walilolitakiwa kufanya.
Kwa mara ya kwanza helikopta ya polisi ilionekana ikizunguka angani saa 7.45 mchana, katika eneo hilo katika barabara ya Azikiwe, ambapo pia kulikuwa na bendi ya muziki ikitumbuiza, huku baadhi ya wananchi wakiwa wamevalia vitenge, kanga na T-Shirt vikiwa na maneno yaliyosomeka: Barack Obama Karibu Tanzania - Welcome.
Ilipofika saa 8.30 mchana, lilipita gari aina ya Land Cruiser lililokuwa limebandikwa picha za Rais Obama, huku likitoa vipeperushi na bendera ya Marekani na kutangaza kwa kutumia kipaza sauti kwamba mgeni ameshatua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Tangazo hilo liliamsha umma wa Watanzania ambao kwa wakati wote tangu saa sita mchana walikuwa wamesimama wakimsubiri kwa hamu kiongozi huyo, hivyo kuamka na kusimama maeneo husika kwa ajili ya kumuangalia.
Licha ya kuamsha shauku ya umati wa wananchi, pia polisi waliwatangazia wafanyakazi katika ofisi zilizopo eneo hilo kufunga vioo vya madirisha, kutochungulia madirishani na wale walionekana juu ya maghorofa kuamriwa kushuka.
Kutokana na amri hiyo, shughuli katika ofisi zilizokuwepo eneo hilo zilisimama kwa kuwa wafanyakazi waliamua kutoka ofisini na kujumuika na wananchi wengine waliokuwa wamejipanga barabarani.
Idadi ya wananchi ilikuwa ikiongezeka kila dakika, hususan wale waliokuwa wakishuka kutoka kwenye pantoni kutoka Kigamboni, walikuwa wakijumuika na wenzao na hata wale walioshuka katika boti wakitokea visiwa vya Pemba na Unguja nao walisimama kuangalia.
Ilipotimu saa 9.35 alasiri, msafara wa Rais Obama ulipita eneo hilo, huku wananchi wakipunga mkono na wengine kushoonya vipeperushi.
Baada ya msafara huo kupita kwenda Ikulu, baadhi ya wananchi walisikika wakilalamika kutokana na kushindwa kumshuhudia kiongozi huyo, na hivyo kuishia kuangalia magari tu.
“Tumekaa hapa tangu mchana tunaungua jua, kumsubiri Rais Obama, lakini tumeishia kuangalia aina ya magari tu waliyokuja nayo, kwani hatujamuona hata kidogo,” alisikika akilalamika mmoja wa wananchi waliokuwa kwenye umati huo.
Baada ya msafara huo kupita, wananchi hao walitawanyika na kwenda kutafuta usafiri, huku askari wa usalama barabarani waliokuwa kwenye bajaj wakitumia kipaza sauti kuwashukuru wananchi kwa utulivu mkubwa waliouonyesha.

KESI ZAENDESHWA ‘CHAP CHAP’
Tofauti na ilivyo siku zote, jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, kesi ziliendeshwa mapema na watuhumiwa kurejeshwa mahabusu kwa kile kilichodaiwa kuhofiwa barabara kufungwa.
Watuhumiwa walifikishwa mahakamani hapo saa moja asubuhi na shughuli za mahakama kuanza mapema, ambapo hadi saa 4.30 asubuhi, mahakama hiyo ilibakiwa na watu wachache, wengi wakikimbilia kumwona Rais Obama.
Mbali na mahakamani, katika benki ya NBC iliyopo katika makutano ya mitaa ya Azikiwe na Sokoine, wafanyakazi wa benki walitoka nje muda mfupi baada ya gari kutangaza kwamba Rais Obama ameshawasili.
Kwa upande wa wafanyabiashara ndogo ndogo wanafanya biashara zao eneo la Posta ya Zamani, nao hawakuonekana kukatiza eneo hilo, tofauti na ilivyokuwa siku za nyuma, ambapo walikuwa wakiweka biashara zao kituoni hapo.

MAMIA WAJITOKEZA, WALONGA
Mwandishi Wetu, Jumanne Gude, anaripoti kuwa, mamia ya wananchi jana walijitokeza kumlaki Rais Barack Obama wa Marekani katika eneo la Posta Mpya, wakati akielekea Ikulu, Dar es Salaam.
Katika barabara ya Kivukoni Front, eneo la Posta Mpya, ulinzi ulikuwa umeimarishwa, ambapo mbwa wa askari wa Marekani walitumika kukagua magari.
Aidha, kulikuwa na utulivu mkubwa kutoka kwa wananchi waliojitokeza katika mapokezi hayo, huku bendi ya matarumbeta ikiwa inatoa burudani.
Ilipofika saa nne asubuhi, shughuli  katika eneo hilo zilisimama kwa muda kutokana mamia ya wananchi kutaka kumwona Rais Obama.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi waliotoa maoni yao kuhusu ujio wa Rais Obama, wamesema wanaamini kuwa ujio wa kiongozi huyo utakuwa na manufaa makubwa kwa Tanzania.
Mohamed Kangulu ambaye alijitokeza eneo la Posta Mpya alisema ujio huo utakuwa na faida kubwa endapo mikataba mbalimbali itakayotiwa saini baina ya nchi mbili hizo itatekelezwa ipasavyo na serikali zote.
“Tumeambiwa kuwa atatia saini mikataba ya miradi ya maendeleo ambayo itakuwa ni ukombozi kwa wananchi kiuchumi, hususan katika suala la umeme,” alisema.
Naye Geogre Mhando alisema anaamini ujio wa Obama utakuwa na manufaa kwa Watanzania wote badala ya watu wachache.
Alisema ni nadra wa kiongozi wa nchi kubwa duniani kama Marekani kuzuru nchi masikini kama Tanzania, hivyo anatarajia ujio huo ni muhimu kwa mustakabali wa Watanzania, hususan kiuchumi na kijamii.
Mhando alisema watu wasiwe na mitazamo hasi kuhusu ujio huo, kwani Rais Obama kama kiongozi wa dunia anahitajika mahali pengi duniani, hivyo ziara yake nchini ni ‘bahati ya mtende’.
Alisema Tanzania bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali, hivyo ziara ya kiongozi huyo utasaidia angalau kutoa mwangaza kwa changamoto hizo.
Grace Mashalla mkazi wa Kimara, alisema amefurahishwa na ujio wa kiongozi huyo wa Marekani na kuongeza anaiona ziara hiyo kama ‘mgeni njoo mwenyeji apone’.
Anasema anaamini kwamba ziara hiyo itakuwa na manufaa makubwa kiuchumi na kijamii, licha ya kauli za uchochezi za baadhi ya watu wasioitakiwa mema Tanzania.
Grace alisema Tanzania na Watanzania wanapaswa kuichukulia ziara hiyo kwa mikono miwili, licha ya changamoto mbalimbali zinazoikabili nchi na watu wake.
Hata hivyo, alisema Watanzania waichukulie ziara ya Rais Obama na ujumbe wake kama neema ya kipekee, hasa ikizingatiwa kuwa baadhi ya nchi kadhaa zinahoji ujio wake hapa nchini.

HALI ILIVYOKUWA JNIA
Katika eneo la nje ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), mamia ya wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya jiji la Dar es Salaam, walijitokeza kwa wingi kumlaki Rais Barack Obama.
Wananchi walianza kukusanyika nje ya uwanja huo uliopo maeneo ya Kipawa, kuanzia saa mbili asubuhi, na kujikusanya katika vikundi wakiwa na shauku ya kutaka kumuona kiongozi huyo wa dunia.
Idadi ya wananchi katika eneo hilo ilikuwa ikiongezeka kila dakika na hadi kufikia saa sita mchana, nje ya uwanja huo kulikuwa kumefurika mamia ya wananchi.
Kutokana na ujio huo, magari yaliyokuwa yakiingia uwanjani hapo kupeleka abiria yalikuwa hayaruhusiwi kutoka, hivyo abiria waliokuwa wakitoka maeneo tofauti kulazimika kutembea kwa mguu hadi maeneo ya Jet ili kutafuta usafiri mwingine.
Hali ya ulinzi na usalama nje ya uwanja ilikuwa imeimarishwa maradufu, ambapo askari wa kikosi cha mbwa na farasi, upelelezi, usalama barabarani na doria walikuwa imara.
Ilipofika saa 5.45 asubuhi, magari ya abiria yaliyokuwa yakitokea maeneo ya Gongo la Mboto kuelekea mjini, yalizuiwa kupita barabara ya Nyerere na badala yake yalikuwa yakipita barabara ya Segerea, Tabata, Mandela na Uhuru.
Saa 6.15 mchana, wananchi waliokuwa wamejipanga nje ya uwanja huo, walipigwa na butwaa baada ya kuona magari maalumu ya Marekani yaliyokuwa yakielekea uwanja wa ndege ili kuwachukua wageni waliofuatana na Rais Obama.
Magari hayo maalumu yalikuwa na rangi nyeusi na muundo wa kipekee na kuwafanya wananchi wengi kuyashangaa.
Ilipofika saa 8.20 mchana, barabara yote ya Nyerere ilikuwa nyeupe na hakukuwa na gari lolote lililokuwa likipita katika barabara hiyo.
Wananchi walijipanga barabarani kuanzia nje ya uwanja wa ndege hadi maeneo ya Tazara, ambapo kila mmoja alikuwa na shauku ya kumuona Rais Obama.
Shughuli mbalimbali za kijamii, hususan biashara za Wamachinga, zilisimama kwa muda kutokana na wananchi wengi kujipanga mstari kando kando mwa barabara hiyo.
Majira ya saa 8.35 mchana, ndege ya Air Force One iliyombeba Rais Obama na mke wake Michelle, ilitua katika uwanja huo na hivyo kuamsha shangwe na vifijo kutoka kwa Watanzania waliofika maeneo hayo kumlaki mgeni huyo na ujumbe wake.
Baada ya wananchi kuiona ndege hiyo, waliingiwa na kiwewe cha furaha na kila mmoja alikaa eneo ambalo angemuona kwa urahisi Rais Obama wakati akipita.
Mara baada ya kuwasili, Rais Obama akiwa na mwenyeji wake Rais Jakaya Kikwete walipigiwa nyimbo za mataifa yaona mizinga 21, na kisha Rais Obama kukagua gwaride la heshima lililoandaliwa na askari wa kikosi cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).
Baada ya shughuli hiyo, Rais Obama akiwa na Rais Kikwete, walipita kukagua vikundi mbalimbali vya ngoma na kusalimiana na viongozi waliofika kumlaki.
Baadaye msafara wa rais Kikwete ulitangulia kuondoka uwanjani hapo kuelekea Ikulu kwa ajili ya kumpokea Obama, ambapo baada ya muda msafara wa Rais Obama uliondoka uwanjani kuelekea Ikulu.
Magari yaliyombeba kiongozi huyo wa dunia, yaliondoka uwanja wa ndege kwa mwendo wa kawaida ambapo wananchi waliojipanga kumuona walikuwa wakipeperusha bendere za Tanzania na Marekani.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi walishindwa kumuona kutokana na gari alilopanda kuwa na vioo vya kiza

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru