Na Solomon Mwansele, Mbeya
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimeendelea kuibana serikali kuhusu madai ya malimbikizo ya walimu, ambayo sasa yanafikia sh. bilioni 6.
Kimeitaka serikali kuhakikisha inalipa haraka madai hayo ili kuwawezesha walimu kuongeza ari katika utendaji kazi.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, Godfrey Zambi, alimweleza Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana, ambaye yupo katika ziara mkoani hapa kuwa, madai hayo ya walimu yanamkosesha usingizi.
Zambi, ambaye pia ni Mbunge wa Mbozi Mashariki, alisema deni hilo linatakiwa kulipa haraka na serikali ili kuondoa hisia za uhusiano ulioyumba baina ya walimu na CCM.
Kwa upande wake, Kinana, alisema CCM kamwe haiwezi kukaa kimya bila kuwatetea wakati walimu wanaidai serikali kiasi kikubwa cha fedha zao, lazima zilipwe haraka.
Alisema tayari CCM imeiagiza serikali kuhakikisha kero zote za walimu zinapatiwa ufumbuzi tena kwa wakati.
“Walimu ni kundi kubwa katika utumishi wa umma, wenyewe ni zaidi ya asilimia 60 ya watumishi wote wa serikali, ni vyema mlitambue kabisa.
“Kero zao zinapaswa kupatiwa ufumbuzi kwa haraka ili wafanye kazi zao kwa ufanisi na kuleta tija kwa taifa,” alisema Kinana.
Pia, alionyesha kushangazwa na madeni ya walimu kuachwa kuwa makubwa, ambapo alisema madeni yao hupatiwa ufumbuzi na baadaye hurundikana tena na kufikia mabilioni ya shilingi.
“Unaweza kukuta madeni yanafikia hadi sh. bilioni 50 na serikali inayahakiki na kulipa, lakini katika kipindi kifupi huanza kurundikana tena na kuzua migogoro,’’ alisema.
Hata hivyo, alisema hilo linapaswa kuepukwa na tayari Rais Jakaya Kikwete, alitoa agizo la walimu kutohamishwa bila kulipwa stahili zao, kama hakuna fedha za kumlipa asihamishwe.
Kurejea kwa malimbizo ya walimu inaashiria kuwa agizo hilo halifanyiwi kazi na baadhi ya watendaji hususan kwenye halmashauri, ambako matatizo mengi huanzia.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru