NA SELINA WILSON
SAKATA la Mbunge wa Arusha Mjini kupitia CHADEMA, Godbless Lema, kuchafuliwa kwenye mitandao, limezidi kuzua sintofahamu, baada ya kushindwa kuwasilisha vielelezo kwa Ofisi ya Bunge.
Hali hiyo imejitokeza baada ya Lema kuomba Ofisi ya Bunge, ishughulikie sakata ya kuchafuliwa kupitia picha zilizosambazwa kwenye mitandao ya simu za kiganjani na ya kijamii.
Akizungumza na Uhuru, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas Kashilillah, alisema ofisi yake ilipokea barua ya Lema, aliyomwandikia Spika wa Bunge, Anne Makinda, akiomba bunge lishughulikie suala hilo.
Alisema Spika Anne alimpatia yeye alishughulikie, ambapo alimwandikia barua Lema ili atoe maelezo ya ziada kwa kuwa, aliyoyatoa awali yalikuwa hayajitoshelezi.
Hata hivyo, licha ya kuandikiwa barua rasmi kuombwa maelezo hayo, Lema hajawasilisha maelezo hayo wala vilelezo vyovyote kwa siku kadhaa tangu alipotakiwa kufanya hivyo.
“Lema aliwasilisha maombi hayo wakati wa vikao vya Bunge mjini Dodoma, vilivyomalizika hivi karibuni, lakini hadi sasa hajawasilisha maelezo ya ziada, hata namba za simu za watu anaowataja amezitoa kwenye vyombo vya habari, lakini sisi hajatupatia.
“Kulingana na utaratibu na kanuni, mbunge yeyote anapokuwa bungeni anakuwa na kinga, na kwamba suala hili lilitokea wakati wa vikao vya bunge, hivyo alimwandikia Spika ili lishughulikiwe na Bunge, lakini hatujaanza kufanya lolote kwa sababu hiyo,” alisema.
Alisema wanahitaji maelezo ya ziada ili wafanye uchambuzi wa jambo lenyewe na kulipima kama ni jinai ili likashughulikiwe na polisi, na kama linahusu bunge, basi lishughulikiwe kwa mujibu wa utaratibu.
Picha zinazomwonyesha Lema, akifanyiwa vitendo vya udhalilishaji, zilisambaa kwenye mitandao wiki iliyopita, ambapo wasambazaji walizituma picha hizo kwenye simu ya mkewe, ambapo zilionwa na mtoto wake mwenye umri wa miaka saba.
Akizungumzia picha hizo, Lema alisema mkewe baada ya kuziona, alimtumia Mbunge wa Iringa Mjini (CHADEMA), Mchungaji Peter Msigwa ili zimfikie yeye.
Kutokana na picha hizo kusambaa, wiki hii Lema alinukuliwa na vyombo vya habari akilalamikia kuchafuliwa kwenye mitandao, na kuomba bunge limsaidie kumsafisha, akielezea kwamba picha hizo zimelenga kumchafua kisiasa .
Lema alitaja namba za simu ambazo zimetumika kusambaza picha hizo na kuchapishwa magazetini, huku akiwatuhumu baadhi ya wanasiasa kwamba ndio wanaomchafua.
Juzi Lema, alitoa kisanga cha mwaka, baada ya kutaka kuonyesha picha hizo kwenye mkutano wa hadhara kabla ya kukataliwa na wananchi waliohudhuria mkutano huo uliofanyika katika viwanja vya mabasi yaendeayo Mburuma wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru