Thursday 14 November 2013

Kinana: Wakulima wa korosho mtalipwa


NA SULEIMAN JONGO, Tandahimba
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana, amewahakikishia wananchi wa mkoa wa Mtwara kuwa, watalipwa malipo yao ya awamu ya pili ya zao la korosho kama wanavyodai.

Kinana amesema atakutana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda ili kuhakikisha wanashughulikia suala hilo la malipo.
Amesema Kamati Kuu ya CCM ilishatoa maagizo ya malipo ya wakulima wa korosho pamoja na kutatuliwa kwa changamoto nyingine za wakulima wa zao hilo, hivyo lazima aelezwe hatua ambazo zimefikiwa na serikali.
Kinana alitoa kauli hiyo jana wakati alipozungumza na wananchi wa kijiji cha Mkwiti wilayani hapa, ambapo alisema umefika wakati kwa wakulima wa zao hilokulipwa fedha wanazodai kama malipo ya pili.
Alisema katika kulisimamia suala hulo, anatarajia kukutana na Pinda na Dk. Kigoda ili kuona namna ya kumaliza kadhia hilo.
ìTunataka kuona hili linafika mwisho badala ya kila siku kusikia wakulima wanalalamika kutolipwa malipo ya awamu ya pili ya korosho zao. Hivyo hili niachieni nitalitafutia ufumbuzi wake,î alisema Kinana.
Hata hivyo, Kinana wakati anazungumzia hilo la malalamiko ya wakulima wa korosho, alisema tayari Kamati Kuu ilishatoa maagizo kwa serikali kuhakikisha inashughulikia changamoto za wakulima hao, huku akiweka wazi kuwa Chama kipo makini katika kufuatilia na kutatua kero za wananchi.
Akizungumzia viwanda vya kubangua korosho, Kinana alitoa maagizo ya kunyangíanywa viwanda hivyo kwa wawekezaji walioshindwa kuviendeleza na badala yake kuvigeuza kuwa maghala ya kuhifadhia mazao.
Alisisitiza kuwa walioshindwa kuviendeleza viwanda hivyo wanyangíanywe na kupewa watu wenye wenye uwezo wa kuviendeleza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilayani hapa, Abdulrahman Namtula, alisema changamoto kubwa ya wakulima ni kutolipwa malipo ya korosho ya awamu ya pili ambayo ni ya mwaka jana.
Alisema kutokana na hali hiyo wana wasiwasi kuwa mwaka huu mazao yatakosa sehemu ya kuhifadhiwa kwa kuwa mazao ya mwaka jana bado yapo ghalani.
Wakati huo huo, Kinana akiwa wilayani Masasi, aliahidi kujenga jengo la CCM wilayani humo ambalo lilichomwa moto kutokana na vurugu zilizotokea mapema, mwaka huu, wakati wananchi walipokuwa wakishinikiza gesi iliyogundulika mkoani Mtwara isisafirishwe kwenda mkoani Dar es Salaam.
ìTutaleta mtaalamu wa kufanya tathmini ndani ya wiki mbili zijazo kuanzia leo, na tutajenga jengo hili upya ili Chama kiweze kuwa na ofisi kama awali,î alisisitiza Kinana.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru