Tuesday 19 November 2013

CCM inafuatilia kwa karibu kero za walimu


NA SULEIMAN JONGO, SONGEA
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimesema kinasubiri utekelezaji wa maagizo yake kwa serikali kuhusu sekta ya elimu, ikiwemo kero za walimu.
Imesema Chama hakiwezi kufumbia macho kuchezewa kwa maslahi ya walimu kwa kuwa, kufanya hivyo ni sawa na kucheizea serikali.
Kauli hiyo alitolewa jana, mjini hapa na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, wakati akizungumza na walimu wanafunzi wa vyuo vikuu na vyuo vya elimu.
ìWalimu ni asilimia 68 ya watumishi wote wa serikali, hivyo kucheza na walimu ni sawa na kuichezea serikali inayoundwa na CCM,î alisema Kinana.
Alisema CCM inafuatilia kwa karibu mwenendo wa serikali katika kushughulikia changamoto za walimu, ikiwemo kulipwa maslahi na kuwekwa sawa kwa utaratibu wao wa ajira.
Akiwa ziarani kwenye mikoa ya Kanda ya Ziwa, alitoa miezi sita kwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kuhakikisha inatatua changamoto za walimu na sekta ya elimu kwa jumla.
“Bado tunasubiri ripoti na utekelezaji wa agizo hilo, baada ya hapo tutajua cha kufanya, lakini kwa hili hatuna mzaha tutalifuatilia kwa karibu kwa kuwa hatuko tayari kulaumiwa kutokana na kasoro za baadhi ya watu tuliowapa madaraka,” alisema.
Kinana alisema anakerwa na vitendo vya dharau vya kutowalipwa kwa walimu, licha ya umuhimu wao kwa taifa.
“Tunaweza kuendesha nchi bila ya baadhi ya watumishi, lakini si walimu, bila wao taifa litaangamia kielimu.
“Tunasubiri muda tuliotoa, endapo utamalizika bila kufanyika kile tulichoelekeza tutatumia njia sahihi za kisheria, ikiwemo kuwatumia wabunge wetu kuwango’a wote walioshindwa kutimiza Ilani ya Uchaguzi ya CCM,” alisema.
Wakati huo huo, Kinana amemwagiza Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Said Mwambungu, kufuatilia na kukomesha vitendo vya udhalilishaji na unyanyasaji wanavyofanyiwa wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph mjini hapa.
Aidha, alimwagiza, Katibu wa NEC, Siasa na Uhusiano wa Kimataifa, Dk. Asha-Rose Migiro, kushughulikia masuala ya ubadilishaji wa kozi na mitaala ya chuo bila kuzingatia mfumo wa Tume ya Vyuo Kikuu nchini (TCU) unaoathiri taaluma nchini.
Katibu mkuu alisema, nakala za malalamiko ya walimu na wanafunzi yatapelekwa TCU na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi ili waeleze namna chuo hicho kinaendeshwa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru