Friday, 8 November 2013

Wachina kizimbani kwa meno ya tembo


NA FURAHA OMARY
RAIA watatu wa China, wanaodaiwa kukamatwa na shehena ya meno ya tembo Mikocheni, Dar es Salaam, wamepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kukutwa na vipande 706 vya nyara hizo zenye thamani ya zaidi ya sh. bilioni tano, mali ya serikali.

Washitakiwa hao, Huang Gin (50), Xu Fujie (22) na Chen Jinzhan (31), wakazi wa Mtaa wa Kifaru, Mikocheni ‘B’, walipandishwa kizimbani jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Gin na wenzake walitangazwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, kukamatwa na nyara hizo katika mtaa huo.
Walisomewa shitaka hilo na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Faraja Nchimbi, akishirikiana na Wakili wa Serikali, Keneth Sekwao, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Mfawidhi, Isaya Arufani.
Hata hivyo, washitakiwa hao hawakutakiwa kujibu lolote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza shauri hilo kwa kuwa husikilizwa na Mahakama Kuu ya Tanzania.
Akiwasomea shitaka hilo kwa lugha ya Kiingereza huku wakitafsiriwa na mmoja wa ndugu wa washitakiwa ambaye ni raia wa China, Nchimbi alidai washitakiwa walitenda kosa hilo, Novemba 2, mwaka huu.
Nchimbi alidai washitakiwa kwa pamoja walikutwa na nyara za serikali, ambazo ni vipande 706 vyenye uzito wa kilo 1,880 ambavyo vina thamani ya sh. 5,435,865,000 mali ya Serikali ya Tanzania, bila ya kuwa na kibali kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori.
Baada ya kusomewa shitaka hilo, Hakimu Arufani alisema mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza ndiyo maana washitakiwa hawakutakiwa kujibu lolote kwani husikilizwa na Mahakama Kuu ya Tanzania.
Hakimu Arufani alisema washitakiwa hao kama wanataka dhamana wawasilishe maombi Mahakama Kuu. Wakili Nchimbi alidai upelelezi unaendelea hivyo anaomba tarehe nyingine ya kutajwa.
Kwa upande wa mawakili wa utetezi, Edward Chuwa na Peter Camillius, walidai watawasilisha maombi ya dhamana Mahakama Kuu. Washitakiwa hao walirudishwa rumande hadi Novemba 21, mwaka huu, kesi itakapokuja kwa kutajwa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru