Thursday 14 November 2013

CCM kumfikisha kizimbani mdeni

Na Latifa Ganzel, Morogoro
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) wilaya hapa, kinakusudia kuifikisha mahakamani Kampuni ya Gwami Investment kutokana na deni la pango linalokadiriwa kufikia sh. milioni 36.

Katibu wa CCM wilayani hapa, Ali Issa Ali, alisema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, baada ya kukabidhiwa jengo ililokuwa imepangishwa kamouni hiyo.
Alisema kampuni hiyo ilikuwa mpangaji kwenye jengo lenye vyumba 24 kwa ajili ya biashara ya nyumba ya kulala wageni tangu mwaka 2007, na kwamba baadaye ilitaka kubadilisha biashara kuwa zahanati.
ìAlipotaka kubadilisha biashara, tulishindwana kwa sababu ni lazima apate idhini kutoka kwetu, na sisi lazima tulijulishe baraza la wadhamini, hivyo tulikuwa hatujaafikiana,î alisema.
Ali alisema mwaka juzi, kampuni hiyo ilitaka kubadili biashara hiyo na ilipokataliwa ndipo ilipoanza kusuasua katika kulipa kodi, hivyo CCM kumwandikia barua za mara kwa mara ikimtaka kulipa deni lake.
Baada ya Chama kuona deni linazidi kuwa kubwa, huku mpangaji huyo akishindwa kulipa kodi hiyo, waliamua kutumia dalali wa mahakama, Property Internation Limited ili waweze kumfuatilia.
Alisema kuwa dalali huyo kwa kushirikiana na CCM waliamua kufikisha suala hilo katika baraza la ardhi la mahakama ya wilaya ili waweze kurejeshewa jengo lao na kupangisha mpangaji mwingine.
Alisema pamoja na kukabidhiwa jengo hilo, bado CCM inakusudia kumfikisha mahakamani Gwami ili aweze kulipa kiasi hicho cha fedha anazodaiwa kama kodi ya pango hilo alilolimbikiza kwa muda wa miaka miwili.
Kwa upande wake, dalali wa mahakama, Calvin Kessy, alisema Oktoba 28, mwaka huu, baraza hilo lilitoa notisi kwa mpangaji huyo kurejesha jengo hilo.
Alisema kuwa baada ya siku 14 ambazo zilitolewa na baraza hilo kumalizika dalali huyo aliamua kuvunja milango ya vyumba vya mpangaji huyo ili kukabidhi jengo hilo kwa CCM.




Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru