Wednesday, 27 November 2013

Mtumishi CRDB afa ajalini


NA JUMANNE GUDE
WATU wawili wamekufa jijini Dar es Saalam, katika matukio tofauti, likiwemo la mfanyakazi wa CRDB, Emmanuel Masanyuti, aliyekufa katika ajali ya gari baada ya kupinduka katika barabara ya Mandela.
Kamanda wa Polisi Mkoa Kipolisi wa Temeke, Anglibert Kiondo, alisema tukio hilo lilitokea jana, saa 6.30 usiku, karibu na mlango wa kuingilia katika Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA).
Kiondo, alisema Masanyuti anayekadiriwa kuwa na umri kati ya miaka 30 hadi 35, alikuwa akiendesha gari yenye namba za usajili T969 BJT, aina ya Toyota Corolla, iliyokuwa inatoka Vetenary kuelekea mataa ya TAZARA.
Alisema gari ilimshinda na kuacha njia ambapo lilipanda tuta kisha kugonga taa za barabarani na hatimaye kupinduka na kusababisha kifo cha mtu huyo.
Kamanda Kiondo, alisema maiti imehifadhiwa katika Hospitali ya Temeke na upelelezi unaendelea ili kubaini chanzo cha ajali hiyo.
Katika tukio lingine, msukuma mkokoteni aliyetambulika kwa jina moja la Mashaba amekutwa amekufa katika eneo la Jangwani Minazi Mirefu.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Marietha Minangi, alisema mwili marehemu ulikutwa juzi, saa 4.00 asubuhi katika eneo hilo ukiwa umelala bila ya kuwa na jeraha lolote.
Kwa mujibu Marietha, marehemu enzi ya uhai wake alikuwa mnywaji wa pombe haramu aina ya gongo, hata hivyo, chanzo cha kifo chake bado hakijafahamika.
Alisema maiti imehifadhiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, ambapo upelelezi unaendelea ili kubaini chanzo cha kifo chake.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru