Wednesday 27 November 2013

Mhariri Uhuru afariki dunia


NA MWANDISHI WETU
MHARIRI Mwandamizi wa magazeti ya Uhuru na Mzalendo, Dunia Mzobora, amefariki dunia.
Mzobora (49), alifariki dunia ghafla leo saa 12 asubuhi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), alikokuwa amepelekwa kwa matibabu zaidi, akitokea Hospitali ya Aga Khan pia ya Dar es Salaam.

Mussa, mdogo wa marehemu, alisema jana kuwa Mzobora alianza kujisikia vibaya juzi usiku akiwa nyumbani kwake, Tabata Mawenzi na kupelekwa Aga Khan, lakini hali ilizidi kuwa mbaya na ndipo alipopelekwa Muhimbili.
Alifariki muda mfupi baadaye wakati madaktari wakiwa katika harakati za kuokoa maisha yake.
Mzobora, ambaye hadi anafariki dunia alikuwa Naibu Msanifu Mkuu wa Uhuru, alifanya kazi hadi kumalizika kwa gazeti la Uhuru toleo la jana, akikaimu nafasi ya msanifu mkuu, akiwa buheri wa afya.
Taarifa zilizopatikana jana kutoka kwa ndugu wa familia, zilisema maziko ya marehemu yatafanyika leo jijini Dar es Salaam.
Mzobora, ambaye alizaliwa Aprili 6, 1964 Mwandiga mkoani Kigoma, alijiunga na Uhuru Publications Limited mwaka 1989, akiwa mwandishi wa habari mwanafunzi, baada ya kumaliza masomo ya ualimu ngazi ya cheti kutoka chuo cha Kasulu, mkoani Kigoma.
Kutokana na uwezo wake na kujituma kazini, mwaka uliofuata alithibitishwa kazini na kupandishwa cheo kuwa mwandishi kamili wa habari.
Mwaka 1992, alipandishwa cheo na kuwa msanifu kurasa wa Mzalendo na Burudani chini ya Msanifu Mkuu wa magazeti hayo kwa wakati huo, Hamisi Mkwinda, kabla ya kupandishwa na kuwa mwandishi wa habari daraja la pili mwaka 1994.
Mwaka 1995, alijiunga na kilichokuwa Chuo cha Uandishi wa habari cha Nyegezi (sasa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine), Mwanza na kuhitimu stashahada ya juu ya uandishi wa habari mwaka 1998.
Baada ya kurejea kazini, alipandishwa vyeo ngazi mbalimbali kuanzia mwandishi mwandamizi daraja la pili na hadi kufariki dunia kwake, alikuwa Mhariri Daraja la Pili.
Miongoni mwa nyadhifa alizoshika ni pamoja na Kaimu Msanifu Mkuu wa Uhuru, Kaimu Mhariri wa Mzalendo na Kaimu Mhariri wa Makala.
Kutokana na kiu yake ya kupenda elimu, mwaka 2006, Mzobora alijiunga tena na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Mwanza kwa masomo ya shahada ya uzamili katika mawasiliano ya umma na uandishi wa habari.
Marehemu ameacha mke na watoto.
Mungu ailaze roho yake mahali pema paponi. Amina.
Wakati huo huo; Rais Jakaya Kikwete, amemtumia salamu za pole Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, kufuatia kifo hicho.
“Nimesikitishwa na kuhuzunishwa na taarifa za kifo cha mmoja wa Waandishi wa habari shupavu na mchapakazi, Dunia Mzobora aliyekuwa akilitumikia Gazeti la Chama Cha Mapinduzi (CCM) la UHURU,” alisema Rais Kikwete.
Alisema alimfahamu Mzobora, enzi za uhai wake, kama Mwandishi wa Habari aliyejituma katika kazi zake za kuuhabarisha, kuuelimisha na kuuburudisha Umma kwa kutumia vyema kalamu yake.
Katika salam hizo, Rais Kikwete ametoa pole pia kwa wafanyakazi wa Kampuni ya Uhuru na Waandishi wote wa habari nchini, kwa kumpoteza mwenzao waliyekuwa wakifanya naye kazi kila siku.
“Aidha, kupitia kwako, naomba unifikishie Salamu zangu za rambirambi kwa familia ya marehemu Dunia Mzobora kwa kumpoteza baba, kiongozi na mhimili wa familia,” alisema Rais Kikwete.
Amewahakikishia wanafamilia kuwa yuko pamoja nao katika kuomboleza msiba wa mpendwa wao, na anamuomba  Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema, aipokee na kuilaza mahala pema peponi Roho ya Marehemu, Amina.
Amewataka wawe na moyo wa uvumilivu, utulivu na subira katika kipindi hiki kigumu wanachopitia baada ya kumpoteza mtu muhimu aliyekuwa kiungo cha familia yao, kwani yote ni mapenzi yake Mola.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru