Saturday 23 November 2013

JK: Teteeni nchi badala ya kuiponda kwenye mablogu


NA MWANDISHI WETU
RAIS Jakaya  Kikwete amesema wajibu wa Watanzania wanaoishi nje ya nchi ni kuisemea vizuri, kuihangaikia na kuitetea nchi badala ya kushinda kwenye mablogu wakiiponda, kuibeza na kulalamika.
Aidha, amesema kuishi kwa Watanzania nje ya nchi kutaonekana jambo la maana zaidi ikiwa watatumia rasilimali na fursa wanazozipata ugenini kusaidia kubadilisha hali na maisha ya ndugu zao waliobakia nyumbani.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Ikulu, Dar es Salaam, Rais Kikwete pia amewaonya Watanzania hao wasije kuchanganyikiwa na kujichanganya kwa kuiga utamaduni wa kigeni kupita kiasi.
Rais Kikwete alikuwa anazungumza na Watanzania waishio Poland. Alhamisi, wiki hii kwenye Hoteli ya Bristol mjini Warsaw ambako alifikia wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku nne.
“Matumaini na matarajio yetu sisi tuliobakia nyumbani ni kwamba mtaisemea vizuri nchi yetu, mtaitetea, mtaihangaikia na kuleta faida nyumbani. Ni jambo ambalo haliingii akilini kuwa baadhi yenu mnaweza kuishi hapa na kazi yenu ikawa ni kushinda kwenye mablogu mkilaumu nchi yenu wenyewe. Nchi mbaya, viongozi hawafai, mnapata faida gani. Mnazo nchi ngapi?, alihoji.
Aliongeza kuwa:  “Kuhangaikia nchi yetu ni wajibu wenu ambao hamwezi kuukwepa. Matumaini yetu ni kwamba mtasukuma mbele maslahi ya nchi yenu, mtatetea ustawi wa nchi yenu na ndugu zenu. Fursa zilizoko hapa mnazijua wenyewe, sisi hatuzijui. Nyie ndio mnaishi hapa, sisi tuko mbali na hatuwezi sisi kutegemewa na kutarajiwa tufanye mambo ya hapa ambayo hatuyajui.”
“Mbona kazi za NGO mnazifanya vizuri bila kusukumwa au kushawishiwa lakini kazi za kusaidia ndugu zenu hamfanyi? Hata kama hamuwezi kusaidia ndugu zenu mnachangia nini nchi yenu?” alihoji.
Rais alisema kwa Watanzania waishio nje kuonekana wanajali na kutetea nchi yao kutasaidia kujenga hoja ya msingi kuhusu umuhimu wa kuanzishwa kwa uraia pacha ambao Watanzania waishio nje wanaulilia.
Kuhusu ombi lao la uraia pacha, Rais Kikwete alisema ni wajibu wa Watanzania waishio nje kuongeza kasi ya kuchangia mjadala kuhusu suala hilo ili likubaliwe kuingizwa kwenye Katiba Mpya.
“Rasimu ya kwanza ya Katiba ilikataa jambo hilo kwa sababu halina ushabiki na upenzi mwingi nyumbani. Ujumbe wangu kwenu jipangeni vizuri kutetea hoja hii. Saidieni mjadala wa jambo hilo badala ya kushinda kwenye mablogu mkijadili siasa na kusahau mambo yenye maslahi kwenu.”
Akizungumzia kuiga utamaduni wa nchi zingine na kusahau wa nyumbani, Rais Kikwete aliwaambia kuwa inaelekea baadhi yao wamejichanganya na kuchanganyikiwa kiasi cha kusahau mambo ya kwao.
Rais Kikwete alitoa kauli hiyo baada ya mmoja wa Watanzania kudai kuwa suala zima la mahari limepitwa na wakati na kuwa kutoa mahari ni sawa ni kuwauza watoto wa kike.
Rais ambaye alionyesha kushangazwa na kauli hiyo, alijibu: “Msiige mambo ya kigeni kiasi cha kuanza kuchanganyikiwa.”

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru