Saturday, 30 November 2013

Sumaye: Wasomi msikae kimya


NA MWANDISHI WETU, Morogoro
WAZIRI Mkuu mstaafu Frederick Sumaye amesema umefika wakati kwa wasomo kushirikikikamilifu katika masuala yanayohusu nchi badala ya kuwaachi wanasiasa tu.
Sumaye alitoa changamoto hiyo jana katika hotuba yake wakati wa uzinduzi wa albam katika Kanisa la Calvarian mjini Morogoro.
Alisema kuwa msomi ni sifa muhimu hasa kama mtu atafanya yale yanayotegemewa na usomi wake na kuwa msomi maana yake ni mwelewa na ana taaluma fulani aliyosomea na bila shaka umebobea katika fani hiyo.
“Kwa kuwa msomi una uwezo wa kuona mbele ya huko tunakoelekea kama tunaenda sawa au la hasa kama jambo lenyewe liko katika fani yako. Ukiwa msomi una nafasi kubwa ya kushauri kwa kutumia utaalamu wako na elimu yako bila uwoga kwa sababu una uhakika na unayoyasema,” alisema Sumaye.
Aliongeza kuwa mtu akiwa msomi ana nguvu kubwa zaidi ya kushawishi kwa sababu atatumia nguvu ya hoja, hivyo sio vizuri msomi akawa mtazamaji na mlalamikaji tu kama wale ambao upeo wao wa kuona na kuchambua mambo ni mdogo.
“Usomi unaheshimika hasa pale mtakapotoa uchambuzi na ushauri wa kitaalamu ambao unasimamia misingi ya taaluma na siyo ya chuki, uhasama, upendeleo au urafiki. Kama rafiki yako akikosea, taaluma haisemi umpongeze bali inataka umshauri kwa kumrekebisha, na vivyo hivyo, kama adui yako au ambaye humpendi akisema kilicho sahihi taaluma inataka uungane naye mikono na kama kwa waziwazi huwezi basi hata kimoyo moyo,” alifafanua Sumaye.
Kwa maoni yake, alisema wasomi wa hapa nchini hawajachukua nafasi yao katika nchi na labda hata katika jamii kwa kuwa kuna mambo mengi makubwa yanayotokea, lakini wasomi wamekaa kimya halafu yakiharibika wanatafuta wa kuwanyooshea vidole wakati madhara yake yanawaumiwa wananchi wote.
Sumaye alisema vyuo vikuu hapa nchini vina maprofesa waliobobea wa fani mbalimbali, madaktari wahadhiri na wanachuo wanaoweza kufanya uchambuzi na utafiti ili kuwa na mchango chanya katika jambo lolote lililoko mbele ya nchi au jamii,nafasi ambayo haijatumika ipasavyo na wakati mwingine kuhisi imetumika vibaya.
“Najua hili lina changamoto zake na mara nyingine mnaweza mkagongana au kukwaruzana na wanasiasa. Hayo tusiyaogope kwa sababu kukwaruzana kwa lengo la kujenga ndiyo afya ya jambo lenyewe. Kunyamaza wakati unajua tunavyokwenda sivyo ni kutokutenda wajibu na hilo ni dhambi,” alisema.
Alisisitiza kuwa: “Wasomi lazima mchukue nafasi yenu katika mambo ya nchi na katika jamii. Msiwaachia tu wanasiasa kila kitu na ninyi mkabaki watazamaji na baadaye walalamikaji. Timiza wajibu wako sasa. Wanasiasa pamoja na kwamba si wajinga, lakini usisahau wana tabia ya kuangalia zaidi kipindi cha uchaguzi.”
Pia, Sumaye alisema upungufu wa maadili mema ni tatizo kubwa katika jamii kwa kuwa unaleta matatizo mengine ikiwemo rushwa, ufisadi, ujambazi, biashara na matumizi ya dawa za kulevya.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru