Tuesday, 19 November 2013

Mkapa azilipua taasisi za binafsi


NA MOHAMMED ISSA
RAIS mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa, amezitaka taasisi binafsi kuwajibika kikamilifu badala ya kujifungia kwenye hoteli kubwa na kuandaa maandiko ya kuomba misaada.
Alisema taasisi nyingi za kiraia hapa nchini, kazi yake ni kuandaa makongamano, semina, badala ya kutekeleza malengo ya kuanzishwa kwa taasisi hizo.
Mkapa, alisema hayo mjini Dar es Salaam jana, katika kongamano lililoandaliwa na taasisi ya Clb de Madrid na Uongozi Institute, ambapo alisistiza kuwa maendeleo hayapatikani kwa kutegemea misaada.
Lengo la kongamano hilo, ni kutoa fursa kwa viongozi wa Afrika kuchambua upungufu na vikwazo vya maendeleo Afrika na kupendekeza mifumo mbadala itakayoweza kufungua kurasa mpya za mchakato wa maendeleo.
Rais huyo mstaafu, alisema pamoja na kuwa na taasisi nyingi nchini, lakini bado hazitekelezi wajibu wao kama ilivyotarajiwa.
Alisema bado zina wajibu mkubwa wa kuleta mabadiliko katika maendeleo ya nchi, bila kutegemea misaada kutoka kwa wahisani.
Kwa mujibu wa Mkapa, kazi zinazofanywa na taasisi hizo ni kujifungia kwenye mahoteli makubwa na kuandaa maandiko ya kuomba misaada kutoka nje, na kwamba, umefika wakati kwa taasisi hizo kutekeleza wajibu wake ipasavyo badala ya kutegemea misaada ya wahisani.
Naye Rais mstaafu wa Nigeria, Olesegun Obasanjo, alisema ni vyema taasisi zote za kiraia kuhusishwa katika hatua za awali za mipango ya maendeleo, jambo ambalo zitasaidia kusukuma maendeleo ya taifa.
Obasanjo, alisema iwapo itabainika kuwa kuna tatizo la mikataba mikubwa ya nchi ni vyema ikatafutwa taasisi itakayotoa miongozo kwenye sekta ya uwekezaji.
Rais mstaafu wa Boswana, Festus Mogae, alisema mafanikio makubwa yaliyopatikana katika nchi yake yameigwa Ulaya.
Alisema nchi hiyo ni ndogo kuliko Tanzania na Nigeria, lakini imepiga hatua kubwa kutokana na kuiga mafanikio kutoka kwenye nchi nyingine, zikiwemo za Ulaya.
Kwa upande wake Mwenyekiti Mtendaji wa Kampuni za IPP, Reginald Mengi, alisema maoni ya Rais Mkapa na Obasanjo ni mazuri na kuna umuhimu wa kuwa na wataalamu wa kutosha, kwenye sekta za uwekezaji.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru