Wednesday, 20 November 2013

Operesheni tokomeza ujangili mazito yaibuka


NA RABIA BAKARI
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamisi Kagasheki, amesema baadhi ya wabunge walitaka Operesheni Tokomeza Ujangili isitishwe kwa kuwa ilianza kuwagusa.

“Tulianza kuwagusa wenyewe (wabunge)... ndipo kelele zilipoanza, tatizo la ujangili ni kubwa mno, Tanzania kila mtu mtaalamu, kila mtu mjuaji,” alisema Kagasheki.
Alitoa kauli hiyo jana, mjini Dar es Salaam wakati akifanya majumuisho ya kikao kati ya wizara na viongozi wa dini, waliomtembelea kwa ajili ya kujadiliana na kupeana mawazo ya namna ya kupambana ili kuokoa maliasili za nchi, ikiwemo tatizo la ujangili.
Balozi Kagasheki alisema wakati Operesheni Tokomeza Ujangili inaanza, wabunge walitoa mapendekezo mazuri na kusifia kwamba ianze, lakini ilipoanza na kasi yake kuwa kubwa na kuanza kuwagusa, wakapiga kelele isitishwe.
Aliongeza kuwa hoja ya kusitisha operesheni hiyo si kubwa kama ambavyo tatizo la ujangili lilivyo.
“Tembo wanauawa kila siku, watu wanapiga kelele isitishwe kwa sababu ya jambo fulani... lakini ukweli huwezi kuacha tembo wanateketea kwa visingizio hivyo,” aliongeza.
Operesheni hiyo ilisitishwa na bunge kwa madai ya kuwepo ukiukwaji wa haki za binadamu, ambapo Balozi Kagasheki alisema ingawa  kulikuwa na mapungufu, lakini kutokana na umuhimu wa operesheni husika isingepaswa kusimamishwa.
Aliugeukia upande wa mahakama kuwa nacho ni chanzo cha kuzorotesha juhudi za kupambana na ujangili huo nchini, kwani sheria kali zilizowekwa hazifuatwi.
“Sheria inasema vingine, mahakama inafanya vingine, inawavunja moyo wadau na askari wanaopambana na ujangili, ni tatizo kwa kweli,” alisisitiza.
Alisema Tanzania ilikuwa ya kwanza duniani kwa kuwa na tembo wengi, lakini baadaye ikashika nafasi ya pili, ikitanguliwa na Botswana, ila kwa hali ilivyo sasa, huenda isiwepo tena kwenye ramani ya nchi yenye tembo.
Aliongeza kuwa mbuga ya Selous ilikuwa na tembo takriban 55,000, lakini takwimu za hivi karibuni zilionyesha kuwa kuna tembo 15,000, na idadi hiyo huenda imeshuka zaidi siku za hivi karibuni.
“Kwa hali ilivyo, sidhani kama hata ndani ya miaka mitano Tanzania itakuwa na tembo hata mmoja... hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere aliposema tutunze maliasili, si kwa kizazi kijacho, bali kwa dunia nzima, kwani ni zawadi ya pekee tuliyopewa na Mungu, lakini itafika kipindi tutabaki na kumbukumbu za picha,” alisema.
Alitolea mfano kontena lililokamatwa na meno ya tembo siku kadhaa zilizopita Zanzibar ni kitu ambacho kimewatisha wadau walio nje ya nchi, kwamba amepokea barua pepe nyingi kuhusiana na jambo hilo na ujangili kwa jumla.
Viongozi wa dini kwa pamoja, walitoa mapendekezo matatu kwa waziri huyo, kwamba kuwe na ushirikishwaji kwenye mambo ya rasilimali za taifa, uundwaji wa chombo kitakachoshirikisha wizara na viongozi wa dini kwa ajili ya kusimamia rasilimali za nchi na muundo wa utekelezaji wa majukumu hayo.
Aidha, walimkabidhi maoni na mapendekezo juu ya kusimamia rasilimali za nchi, na kumueleza kuwa wamefikia hatua hiyo baada ya kuandaa kongamano lililokuwa na mafanikio, lakini wizara hiyo haikuwa na mwakilishi.
Akijibu hoja hizo, Balozi Kagasheki alikiri kusahau upande wa viongozi wa dini, lakini ukweli wao ndiyo wenye wananchi ambao wanaingia misikitini na makanisani, hivyo wakipata elimu ni rahisi kuelimisha watu wengine.
Alitoa agizo kuwa ndani ya wiki moja, upatikane muafaka wa chombo hicho na muundo wa utekelezaji wake, kwa kuwa wizara na serikali kwa jumla haina tatizo na jambo hilo.
Mkutano huo ulihudhuriwa na wakurugenzi wa idara, watendaji wa ngazi za juu na viongozi wa dini waliwakilishwa na Askofu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Mashariki, Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Stephen Munga, Sheikh Mkuu wa Dar es Salaam, Alhad Salum na watendaji wengine wa kamati ya viongozi wa dini

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru