Thursday 28 November 2013

Maelfu wamzika Mhariri wa Uhuru


Na Mwandishi Wetu
WAANDISHI wa habari kutoka vyombo mbalimbali nchini na watu mbalimbali, jana waliungana katika maziko ya aliyekuwa Mhariri Mwandamizi wa Magazeti ya Uhuru na Mzalendo, Dunia Mzobora.
Mzobora (49), alifariki dunia juzi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa shinikizo la damu, alizikwa jana katika makaburi ya Kisutu mjini Dar es Salaam.
Mbali na waandishi wa habari, maziko hayo pia yalihudhuriwa na mamia ya wananchi, wanasiasa wakiwemo viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Dar es Salaam.
Naye Katibu Mkuu wa CCM Abdulrahaman Kinana na Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi  Nape Nnauye, wamemtumia salama za pole, kwa uongozi, familia na wafanyakazi wa kampuni ya Uhuru Publications Ltd (UPL) kufuatia kifo hicho.
Viongozi hao, walisema wameshtushwa, na na kuhuzunishwa kufuatia kifo.
“Tutaendelea kuuenzi mchango wa marehemu Mzobora ambao aliutoa katika kampuni hii enzi ya uhai wake,” walisema.
Marehemu Mzobora, alianza kujisikia vibaya juzi usiku akiwa nyumbani kwake, Tabata Mawenzi na kupelekwa Aga Khan, lakini hali ilizidi kuwa mbaya na ndipo alipopelekwa Muhimbili, ambapo alifariki muda mfupi baadaye wakati madaktari wakifanya jitihada za kuokoa maisha yake.
Hadi anafariki dunia, alikuwa Naibu Msanifu Kurasa Mkuu wa Uhuru. Alizaliwa Aprili 6, 1964 Mwandiga mkoani Kigoma, alijiunga na Uhuru Publications Limited mwaka 1989, akiwa mwandishi wa habari mwanafunzi, baada ya kumaliza masomo ya ualimu ngazi ya cheti kutoka chuo cha Kasulu, mkoani Kigoma.
Kutokana na uwezo wake na kujituma kazini, mwaka uliofuata alithibitishwa kazini na kupandishwa cheo kuwa mwandishi kamili wa habari.
Mwaka 1992, alipandishwa cheo na kuwa msanifu kurasa wa Mzalendo na Burudani chini ya Msanifu Mkuu wa magazeti hayo kwa wakati huo, Hamisi Mkwinda, kabla ya kupandishwa na kuwa mwandishi wa habari daraja la pili mwaka 1994.
Mwaka 1995, alijiunga na kilichokuwa Chuo cha Uandishi wa habari cha Nyegezi (sasa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine), Mwanza na kuhitimu stashahada ya juu ya uandishi wa habari mwaka 1998.
Kutokana na kiu yake ya kupenda elimu, mwaka 2006, Mzobora alijiunga tena na Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Mwanza kwa masomo ya shahada ya uzamili katika mawasiliano ya umma na uandishi wa habari. Marehemu ameacha mke na watoto.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru