Na Hamis Shimye
UFAULU wa mtihani wa kumaliza darasa la saba kwa mwaka 2013, umepanda kwa masomo yote ikilinganishwa na mwaka jana.
Imeelezwa kuwa ufaulu huo umeongezeka kwa asilimia 19.89 ikilinganishwa na ilivyokuwa kwa mwaka uliopita.
Pia, imeelezwa kuwa somo ambalo watahiniwa hao wamefaulu zaidi katika mtihani wao ni Kiswahili ambapo ufaulu ni asilimia 69.06 huku wakiwa wamefeli zaidi kwenye somo la Hisabati ambalo ufaulu upo chini kwa asilimia 28.62.
Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA), Dk. Charles Msonde alisema wanafunzi 427,606 walifanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2013 huku kiwango cha udanganyifu kikizidi kudhibitiwa hivyo kupungua.
Hata hivyo, alisema NECTA imefuta matokeo yote ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kwa watahiniwa 13, ambao walibainika kufanya udanganyifu. Watahiniwa waliofutiwa mwaka jana ni 293.
Alisema kati ya wanafunzi hao, 844,938 waliofanya mtihani huo wamepata alama zaidi ya 100 katika alama 250.
“Idadi hiyo ni sawa na asilimia 50.61. Kati yao wasichana walikuwa 208,227(sawa na asilimia 46.68) na wavulana 219,379 sawa na asilimia 55.01,” alisema.
Dk. Msonde alisema katika ufanyaji wa mtihani huo, pia walikuwepo watu wenye ulemavu, ambapo wasichana walikuwa 219 na wavulana 257.
Hivyo, alisema matokeo hayo yatapelekwa maeneo yote husika ili mchakato wa upangaji shule ukifanyika kwa watahiniwa wote waliofaulu mtihani huo wa kumaliza elimu ya msingi.
Kuhusu usahihishaji mitihani, Dk. Msonde alisema ili kujiridhisha na usahihi wa zoezi la usahihishaji wa kutumia mfumo wa kompyuta, sampuli za karatasi 20,795 ya majibu ya watahiniwa wa shule 200 kutoka wilaya 48 zilichukuliwa.
Alisema sampuli hizo ni kutoka shule katika wilaya 48 za mikoa tisa ya (Iringa, Kagera, Shinyanga, Manyara, Njombe, Mbeya, Morogoro, Katavi na Tanga) zilisahihishwa kwa mkono.
“Ulinganifu baina ya alama za watahiniwa zilizopatikana kwa kusahihishwa kwa mkono na zile zilizotokana na usahihishaji wa mfumo wa kompyuta ulifanyika na kubaini kompyuta ilikuwa sahihi,”alisema.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru