Na Innocent Ng’oko, Mbeya
WAZIRI wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ameonya kuwa wafanyabiashara wasipotumia vyema fursa ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe, wataugeuza mkoa wa Mbeya na mingine ya jirani kuwa jalala la bidhaa kutoka nje.
Aliwataka kuhakikisha wanatumia ipasavyo fursa ya uwanja huo kukuza biashara na mataifa mengine na kupanua masoko ya bidhaa kwa Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini.
Alisema maonyesho hayo yenye lengo la kufungua mikoa ya Nyanda za Juu Kusini kama fursa ya uwekezaji, hayatakuwa na maana iwapo wafanyabiashara hawatawekeza na kuchangamkia fursa za masoko mapya na kubadilishana mbinu za kibiashara.
Alisema maonyesho hayo yanatakiwa kuwa chachu ya wafanyabiashara, wakulima na wenye viwanda, kujitathimini katika kuzalisha bidhaa zenye ubora zaidi na ambazo zitakidhi ushindani wa kibiashara na mataifa ya jirani yakiwemo ya Kenya, Uganda, Malawi, Zambia na mataifa mengine.
“Unajua maonyesha haya ni muhimu kwa kuwa yanatupa picha ya moja kwa moja na yenye ulinganifu wa bidhaa tunazozalisha na wanazozalisha wenzetu wa nje,’’alisema Dk. Mwakyembe.
Akitolea mfano, alisema Mbeya imejaaliwa kuwa na mazao adimu na yenye ubora yakiwemo maparachichi, viazi vitamu na mviringo, kokoa, kahawa, chai, mpunga na matunda mbalimbali.
Hata hivyo, Dk. Mwakyembe alishitushwa na tabia ya baadhi ya wamiliki na wafanyakazi wa kampuni za kigeni kutumia bidhaa zikiwemo mbogamboga, matunda, ndizi na mchele kutoka nje ya nchi.
Awali, Mwenyekiti wa TCCIA Mkoa wa Mbeya, Lwitiko Mwakalukwa, alisema kusuasua kwa maonyesho hayo kunatokana na kuwepo kwa kongamano kubwa la wafanyabiashara kutoka mataifa mbalimbali, lililofanyika Dar es Salaam.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru