Thursday 14 November 2013

Chiza ashusha bei mbegu za pamba



Na Chibura Makorongo, Simiyu
WAZIRI wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, ametangaza kushushwa kwa bei ya mbegu za pamba zinazosambazwa na Kampuni ya Quton.

Hatua hiyo inatokana na mbegu hizo kulalamikiwa na wakulima kwamba, bei yake ni kubwa. Hivi sasa mbegu hizo zitauzwa kwa sh. 600 kwa kilo moja badala y ash. 1,200.
Uamuzi huo unatokana na malalamiko ya muda mrefu ya wakulima wa pamba kupinga bei ya sh. 1,200 kwa kilo moja badala ya sh. 200 iliyokuwa ikitumika kwa kipindi kirefu, hivyo kufanya wakulima kugoma kutumia mbegu hiyo.
Mbali ya kushushwa kwa bei hiyo, erikali imewaruhusu wakulima kuendelea kutumia mbegu zenye manyoya na kuagiza waachwe waamue wenyewe ni mbegu zipi wanazopenda badala ya kuwalazimisha kama ilivyokuwa imeelekezwa awali na Bodi ya Pamba nchini (TCB).
Akitangaza uamuzi huo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Ngongwa wilayani Maswa, mkoani Simiyu, juzi, Waziri Chiza, alisema kupunguzwa kwa bei ya mbegu hizo kunalenga kuwapa nafuu wakulima wa zao hilo.
Hata hivyo, alisema serikali itatoa ruzuku ya sh. Bilioni 4.8 kwa kampuni hiyo ili kufidia pengo lililojitokeza, huku akiwahimiza wakulima kutumia mbegu hizo baada ya kubainika kuwa bora.
Alisema mbegu zenye manyoya zimetajwa kuporomoka ubora wake kwa kiasi kikubwa, hali inayofanya mavuno ya wakulima kuwa kidogo.
“Bei ya mbegu hizi za Kampuni ya Quton zimeleta kelele, baada ya kukaa na wawakilishi wenu, serikali imekubali bei hiyo iteremshwe na sasa itauzwa kwa sh. 600 badala ya 1,200 kwa kilo moja.
“Serikali yenu imeamua kwa nia nzuri ili muweze kumudu kuendelea na kilimo bila tatizo,” alieleza Chiza huku akishangiliwa na wananchi hao.
Hata hivyo, alisema hakuna sababu za kuwalazimisha wakulima kupanda mbegu za Quton, bali waachwe wenyewe na kwamba watabadilika taratibu baada ya kuona mavuno mengi watakayopata wenzao waliopanda mbegu hizo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru