Friday, 8 November 2013

Ujenzi wa bomba la gesi washika kasi


NA SELINA WILSON
KAZI ya kuunganisha mabomba katika bomba kubwa la gesi, imefikia urefu wa kilomita 142 kati ya 542 kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam.
Kazi hiyo ambayo ilianza Septemba 26, mwaka huu, inafanywa na vikosi sita vilivyoko katika maeneo mbalimbali ikiwemo Somanga Fungu ambako bomba litapita chini ya bahari umbali wa kilomita 25.

 Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, alitoa taarifa hiyo jana katika ziara ya kukagua ujenzi wa bomba hilo iliyowahusisha wadau wa maendeleo wakiwemo wa Benki ya Dunia (WB).
Maswi alisema kutokana na kasi ya ujenzi huo, wanatarajia kukamilisha Julai mwakani na kuwa ujenzi wa kiwanda cha kusafisha gesi utakuwa umekamilika Desemba, mwakani, ambapo shehena ya kwanza ya gesi itafika Dar es Salaam.
Alisema kazi ya kuunganisha mabomba inafanywa kwa utaalamu wa hali ya juu na kuwa yanaunganishwa yakiwa maeneo ya kuchimbiwa.
Kwa upande wa mabomba yatakayopita baharini, alisema watatumia reli maalumu kwa ajili ya kupeleka mabomba yaliyoongezewa uzito kwa kutumia zege.
Maswi alisema lengo la  ziara hiyo kwa wadau wa maendeleo ni kuwaonyesha  ujenzi unavyoendelea kwa kuwa wengi walikuwa wakipinga na kutoamini kama itawezekana na wengine wakidhani wajenzi wa Kichina watalipua ujenzi huo.
“Baada ya kutembelea wameshuhudia ujenzi kwa kutumia utaalamu wa kisasa huku mshauri mwelekezi akieleza kuwa bomba hili ni la kisasa kuliko mabomba mengine ya gesi asilia,”alisema.
Maswi alisema ujenzi wa bomba hilo unaenda sambamba na  ule wa kituo cha kuzalisha umeme cha Kinyerezi I unaotarajiwa kukamilika Agosti, mwakani.
Alisema  ujenzi wa kituo kingine cha Kinyerezi II wa megawati 240 unatarajiwa kuanza na utakamilika baada ya miezi 18.
Akizungumza katika eneo la kuunganisha mabomba yatakayotandikwa chini ya bahari, Mshauri Mwelekezi wa Kampuni ya Worley Parsons, Pieter Erasmus, alisema yanayoongezewa uzito toka tani tano hadi 11 ili kuyaimarisha.
Kwa upande wake, mhandisi wa bomba hilo kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Bartazar Mrosso, alisema ujenzi unaendelea kwa kasi na kwamba baada ya kumaliza kuunganisha bomba, kazi itakayofuata ni kuchimba mtaro na kulitandika na kuwa hadi Julai, mwakani kazi hiyo itakuwa imekamilika.
Ujenzi wa bomba hilo ulianza Agosti 15 mwaka huu, ulipangwa kukamilika ndani ya miezi 18. Ujenzi huo unagharimu sh. trilioni 1.9 ambazo ni mkopo kutoka Benki ya Exim ya China.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru