NA MWANDISHI WETU, DODOMA
SERIKALI imesema tatizo la ajira linalowakabili vijana wengi nchini, litamalizwa kwa kukuza uchumi utakaosaidia kutoa fursa za watu kufungua viwanda, kujikita katika kilimo na sekta zingine za uzalishaji mali.
Alisema hakuna kipaumbele katika taifa kuliko kukuza uchumi, kwani kila kipaumbele lazima kijibu maisha ya wananchi, ili kuweza kutoa fursa ya kuguswa nacho moja kwa moja.
Alisema kipaumbele ambacho serikali imezingatia katika mpango huo ni kukuza uchumi, ambapo inaamini kwa kufanya hivyo kutasaidia kuondoa umasikini, kupunguza tatizo la ajira na ukosefu wa huduma duni za afya.
Wasira ambaye alikuwa akijibu baadhi ya hoja za wabunge, waliokuwa wakieleza kuwa serikali imekuwa na vipaumbele vingi kuliko uwezo wa kuvitatua, alisema hakuna kipaumbele kikubwa ambacho serikali imekiainisha zaidi ya kukuza uchumi wa taifa.
ìKama tukikuza uchumi, tunakuwa tunatoa fursa ya viwanda kujengwa, kilimo kuendelea na ukosefu wa ajira utapungua, bila mpango kujibu maisha ya watu unakuwa unafanya kazi bure na majibu pekee ya maisha ya watu ni kukuza kwanza uchumi.
ìNdiyo maana hicho ndicho kipaumbele namba moja, vingine ni vishereheshaji tu, lakini kwanza lazima tuweke miundombinu ya nishati, uchukuzi kwa maana ya reli, bandari, ndege na maji, vyote hivi vinalenga kwanza kukuza uchumi,î alisisitiza.
Wasira alisema kama nishati ipatikana, barabara, reli, viwanja vya ndege vikipatikana vitasaidia wawekezaji kujenga viwanda ambavyo vitazalisha ajira na kupunguza makali ya maisha ya wananchi kwa kupata urahisi wa usafiri.
Pia, alisema kuwa kwa kupata miundombinu ya sekta hizo, kutasaidia mkulima kufanya kilimo cha kisasa kwani atakuwa na uhakika wa kusafirisha mazao yake, soko la mazao yake na hivyo watu wengi wataweza kujikita katika kilimo kwa sababu ya miundombinu bora.
Alisema serikali inatambua kuwa kwa mujibu wa sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012, asilimia 67.1 ya wananchi wote ni vijana wa kati ya umri wa miaka 15 hadi 35, na kwamba kati yao asilimia 13 hawana ajira.
Kwa mujibu wa Wasira, katika kuondoa tatizo hilo, kitu cha kwanza ni kukuza uchumi kutakakofanya sekta zingine kuzalisha nafasi nyingi za ajira na pia kusimamia mtiririko wa utekelezaji wa miradi inayobuniwa na kusimamia nidhamu ya matumizi.
Alieleza kuwa lazima kutatua tatizo la ununuzi ambalo limekuwa likichangia kupotea kwa fedha nyingi za serikali kutokana na soko kuonyesha bei ya chini ya bidhaa, lakini kitengo cha unununzi kikionyesha gharama kubwa.
Aidha, alieleza kuwa mpango wa maendeleo lazima ujibu matatizo ya umasikini wa wananchi, kwani haitoshi kusema uchumi unakua kwa asilimia saba wakati hauna uhalisia wa maisha ya Mtanzania, hivyo ili mpango huo ujibu matatizo ya umasikini lazima tujikite katika kilimo cha kisasa.
Pia, alishauri wasambazaji wa pembejeo za kilimo na mbolea kuwa na utamaduni wa kusambaza vitu hivyo wakati wote wa mwaka kuliko kusubiri msimu na ndipo waanze kuwapelekea wakulima, kitu ambacho huleta usumbufu mkubwa kwa wakulima.
Vilevile, alisema serikali itaendelea na ujenzi wa reli kwenda nchi jirani, hivyo kuwaomba watu wasikalie kulalamika hata kama nchi jirani wanajenga za kwao, kwani hakuna mfanyabiashara ambaye anaweza kusafirisha mizigo kwa reli ya kilomita 200 na kuacha yenye kilomita 125, labda awe anafanya hivyo kisiasa na sio kuingiza faida.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru