Thursday 14 November 2013

NHIF kuwakopesha wadau wake bil. 10/-


Na Nathaniel Limu, Singida
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), umeidhinisha sh. bilioni 10 zitolewe mikopo kwa watoa huduma, ili waweze kununulia vifaa tiba na kukarabati maeneo ya kutolea huduma.
Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya NHIF, Lydia Choma, alisema hayo alipowaeleza wadau mkoani hapa katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Katala Beach Hotel.
Lydia alisema utaratibu huo wa mikopo ya bei nafuu hairejeshwi kwa fedha taslimu, isipokuwa kwa kukatwa katika madai ambayo mtoa huduma anawasilisha katika mfuko.
“Kwa mkopo wa vifaa tiba, huu hurudishwa kwa makato ya asilimia kumi ambayo hulipwa ndani ya miezi 24, na mikopo ya ukarabati wa maeneo ya kutolea huduma ni miezi 36,” alifafanua.
Aidha, Lydia alisema NHIF itaanza kutoa tuzo maalumu kwa halmashauri zitakazoandikisha kaya nyingi katika mfuko huo.
“Menejimenti ya mfuko ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha mapendekezo ya utekelezaji wa mpango huu, na sisi katika bodi, tutayaangalia ili kusudi yawe kichocheo cha kufikia afya bora kwa wote sasa,” alisema mjumbe huyo.
Katika hatua nyingine, Lydia alitumia fursa hiyo kuipongeza halmashauri ya Iramba mkoani hapa kwa kuwa ya kwanza nchini kwa wananchi wake wengi kujiunga na mfuko huo.
Awali, Mkurugenzi wa Takwimu na Uhai wa NHIF, Michael Mhando, aliwaomba viongozi mkoani hapa katika ngazi mbalimbali, wafanye mjadala kuhusu huduma za NHIF na CHF/TIKO, kuwa  ajenda ya kudumu katika vikao vyao vya maamuzi.
« Lengo ni kutatua matatizo katika ngazi ya mkoa yasisubiri maamuzi ya juu ili kutoa taarifa kuhusu utekelezaji wa mpango wa shughuli za NHIF, CHF na TIKA mkoani hapa,” alisema.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru