NA SULEIMAN JONGO, Mbozi
WALIMU wilayani Mbozi katika mkoa wa Mbeya, wameeleza kukerwa na tabia ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Hawa Ghasia ya kuwa mbabe na kukataa kusikiliza kilio chao.
Wamesema waziri huyo hataki kusikiliza matatizo yao na kukaa nao meza moja kwa ajili ya kujadili mambo yanayohusu maslahi yao.
Pia, wamelalamikia kukopwa kwa fedha zao sh. milioni 200 za Chama cha Akiba na Mikopo (SACCOS) wilayani humo zinazodaiwa kutumika kwenye maandalizi ya sherehe za Mei Mosi, mwaka huu, iliyofanyika kitaifa mkoani Mbeya.
Akizungumza katika kikao, Mwakilishi wa walimu wa wilaya ya Mbozi na Momba, Leonard Nyang’uye, alisema wanashangazwa na hatua ya waziri kukataa kuwasikiliza walimu badala ya kuwa msaada katika kutatua kero zao.
Nyang’uye alisema Novemba 13, mwaka huu, waliomba kukutana na waziri ili kuwasilisha malalamiko yao, lakini alikataa kusikiliza kwa madai kuwa serikali imeshamaliza matatizo ya walimu.
“Waziri alimkataza Katibu wa Chama Cha Walimu, Emilia Mwakyoma kusoma taarifa badala yake alimwamuru kukaa chini mara moja kwa madai kwamba matatizo yetu yamekwisha baada ya kushughulikiwa na serikali. Jambo hili lilituumiza kichwa na kutukera walimu. Katibu Mkuu wa CCM tunaomba ufahamu kuwa waziri huyu amekuwa kiburi kwa walimu na siku hiyo alionyesha ukali usio na sababu mbele yetu,” alisema.
Aliongeza kuwa kauli ya Waziri Hawa kwa walimu aliokutana nao siku hiyo iliwafanya washindwe kuwasilisha malalamiko yao na kwamba wamefarijika na ujio wa Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman Kinana, kwa kuchukua hatua ya kuwaita ili kujadili mambo yatakayoweka sawa mustakabali wa maslahi yao.
“Tunaamini utatusaidia kwa kuwa waziri mwenye dhamana ameshindwa kutusikiliza,” alisema mwakilishi wa walimu hao.
Kuhusu madai ya fedha za SACCOS kuliwa na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, walimu walimwambia Kinana kuwa wamekuwa wakifuatilia fedha hizo, lakini wamekuwa wakipewa majibu yasiyoridhisha.
Mwakilishi huyo alisema kila wanapofuatilia wamekuwa wakielezwa kuwa fedha zao zilitumika kwenye sherehe za Mei Mosi.
Alisema fedha zilizoliwa ni zile walizokuwa wakidunduliza na kujiwekea ili kusaidiana angalau kuinua hali zao kimaisha.
Nyang’uye, alisema fedha hizo zilitumiwa na halmashauri yao pasipo kushirikishwa na sasa wamekuwa wakisumbuliwa kila wanapozihitaji.
“Tulipohoji kuhusu fedha zetu tulielezwa kuwa zilitumiwa na uongozi wa Wilaya za Mbozi na Momba kuandaa sherehe za Mei Mosi,” alisema.
Baada ya kusikiliza kilio cha walimu hao, Kinana aliahidi kukifanyia kazi ambapo alisema suala la waziri majibu yake yatatolewa na Rais kwa kuwa ndiye mwenye uwezo wa kufanya hivyo.
“Hili la waziri nimelisikia, ninawaahidi nitakwenda kuonana na wahusika, siwezi kusema hapa tutachukua hatua gani, tutalifikisha kwa utataribu unaoeleweka,” alisema Kinana.
Kuhusu fedha za walimu kuliwa na halmashauri ya wilaya, Kinana alitaka walimu kurudishiwa fedha zao haraka na kwamba katika hilo hataki kusikia linachukua zaidi ya mwezi mmoja.
Kinana alimhoji Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi, Charles Mkombachepa, kuhusu matumizi ya fedha za walimu.
ìMkurugenzi tueleze fedha za walimu hawa zimetumika vipi, ukizingatia kwamba mishahara yao ni midogo na hata hicho kidogo wanachokipata mmekikopa, eti kwa kuandaa Mei Mosi, kwani siku hizi Mei Mosi inaandaliwa na walimu?î alihoji.
Mkurugenzi huyo alikubali kutumia fedha hizo kwa ajili ya kulipia huduma zilizotolewa na taasisi mbalimbali wilayani humo.
Alisema fedha hizo hazikutumika kwa ajili ya Mei Mosi, bali zilitumiwa kuandaa usafiri, kurekebisha magari na
shughuli nyingine zisizohusiana na walimu moja kwa moja.
Mkombachepa aliomba kulipa fedha hizo katika kipindi cha miezi miwili ijayo. Hata hivyo, Kinana alimtaka Mkurugenzi huyo kulipa fedha hizo mara moja.
Saturday, 30 November 2013
Walimu wamshtakia Kinana
06:50
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru