Thursday 28 November 2013

Mzee adaiwa kubaka kibinti, ajitosa majini


Na Mohammed Mhina wa Jeshi la Polisi Zanzibar
MKAZI wa Kijiji cha Kidutani Gando mkoa wa Kaskazini Pemba, Muslih Mserembe, ametiwa mbaroni kwa tuhuma za kumbaka mtoto (jina linahifadhiwa) mwenye umri wa miaka 12 kisha kujitosa bahari kukwepa mkono wa dola.
Mserembe (55), alikamatwa na watu waliokuwa wamekizingira kibanda chake kilichojengwa kwa miti wakati akimbaka binti huyo bila huruma.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa, alisema tukio hilo lilitokea jana saa 12.00 asubuhi wakati binti huyo akiwafuatilia wenzake kwenda shambani kuokota maembe, ndipo mzee huyo alipomuona na kumuita.
Alisema baada ya binti huyo kumsogelea, alimwambia waingie ndani ya nyumba yake akidai kuwa angempatia maembe badala ya kuwafuata wenzake, ndipo alipombaka na binti huyo alipiga kelele za kuomba msaada.
Kamishna Mussa, alisema baada ya kelele hizo majirani walifika nyumbani kwa Msarembe na wakati wakiizingira nyumba yake, alitoka na kutimua mbio na kwenda kujitosa baharini.
Watu hao walimkimbiza nao walijitosa baharini na kumvua kama samaki.
Alisema baada ya kumkamata walimpeleka katika kambi moja ya KMKM ambapo Polisi walifika na kumchukua kwa hatua zaidi.
Kamishna huyo alisema binti aliyebakwa alipelekwa katika Hospitali ya Wete mkoa wa Kaskazini Pemba kwa matibabu zaidi na hali yake imeelezewa kuendelea vizuri.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru