Thursday 28 November 2013

Pinda kuzindua tovuti ya serikali


Na mwandishi wetu
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, anatarajia kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa Tovuti Kuu ya Serikali katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu. Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Uzinduzi wa Tovuti hiyo inayopatikana kwa anuani ya www.tanzania.go.tz, utahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wananchi, wafanyabiashara, washirika wa maendeleo, taasisi zisizo za serikali na wawakilishi kutoka vyuo vikuu.

Imeelezwa kuwa hizo ni juhudi za serikali  katika kuhakikisha kuwa taarifa na huduma inazozitoa zinapatikana na kuwafikia wananchi kwa urahisi.
Taarifa na huduma katika Tovuti Kuu hiyozimegawanywa katika maeneo makuu sita ya serikali, wananchi, taifa, biashara, sekta na mambo ya nje.
Inalenga kutoa huduma mbalimbali kama upatikanaji wa nyaraka zote za Serikali, huduma zinazotolewa na serikali kwa njia ya simu na mtandao, viwango vya fedha, hali ya hewa, na soko la hisa.
Huduma nyingine katika Tovuti Kuu hiyo imetengwa katika ukarasa wa Nifanyeje? ambao  unamjengea uwezo mwananchi wa kufahamu utaratibu wa upatikanaji wa huduma zinazotolewa na taasisi mbali mbali za Serikali.
Inalenga pia kuziunganisha tovuti na mifumo ya taasisi mbali mbali inayotoa taarifa na huduma kwa wananchi na wafanyabiashara katika dirisha moja.
Tovuti Kuu hiyo ilianza kutengenezwa mwaka 2009 na kupatikana kwa anuani ya www.egov.go.tz chini ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma.
Iliboreshwa na kuunganishwa na iliyokuwa Tovuti ya Taifa kwa anuani ya www.tanzania.go.tz mwaka 2012 chini ya Wakala wa Serikali Mtandao.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru