Saturday 30 November 2013

Pangua pangua ndani ya polisi


NA MWANDISHI WETU
JESHI la Polisi limefanya mabadiliko makubwa ambapo limemhamisha aliyekuwa  Kamanda wa Polisi mkoa wa Kagera, Philip Kalangi,  kwenda Makao Makuu, Dar es Salaam.
Pia, mabadiliko hayo yamewagusa baadhi ya wakuu wa upelelezi wa mikoa na wakuu wa polisi wa wilaya.
Katika mabadiliko hayo, Kalangi atakuwa Mkuu wa Kikosi cha Kusimamia Usalama wa Mazingira na nafasi yake itachukuliwa na Kamishana Mwandamizi wa Polisi (SACP), George Mayunga ambaye alikuwa mkuu wa kikosi hicho, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na msemaji wa jeshi hilo, Advera Senso, baadhi ya Wakuu wa Upelelezi wa Mikoa (RCO) na Wakuu wa Polisi wa Wilaya (OCD) waliobadilishwa ni RCO Tabora, (ACP) Edward Bukombe ambaye amehamishiwa Makao Makuu ya Upelelezi Dar es Salaam.
RCO wa Geita, (ACP) Francis Kibona amehamishiwa Mkoa wa Njombe kuwa RCO na nafasi yake itachukuliwa na SSP, Simon Pasua,  kutoka Makao Makuu ya Upelelezi Dar es salaam.
Wengine ni aliyekuwa OCD wa Wangingíombe,  SSP, Francis Maro amehamishiwa Mkoa wa Katavi kuwa RCO na aliyekuwa RCO Katavi, ACP, Emmanuel Nley,  amehamishiwa Kikosi cha Polisi  Wanamaji Dar es Salaam.
Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Rukwa, SSP,  Peter Ngussa amehamishiwa Makao Makuu ya Upelelezi Dar es salaam, nafasi yake inachukuliwa na SSP Alan Bukumbi.
Aliyekuwa Mkuu wa Polisi wilaya ya Kati, Mrakibu wa Polisi (SP) Salum Ndalama, anakwenda kuwa Kaimu Mkuu  wa Upelelezi Mkoa wa Tabora na aliyekuwa OCD wa Tunduru, SP, Amadeus Tesha anakwenda kuwa Mkuu wa Upelelezi Kikosi cha Polisi Reli.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi limezindua bodi ya udhamini wa mfuko wa usalama wa raia utakaosaidia polisi kutekeleza mpango wake wa maboresho katika jeshi hilo.
Mkuu wa Polisi nchini, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) Said Mwema, alisema maboresho yana gharama kubwa, ambapo kwa utekelezaji wa awamu ya kwanza zinakadiriwa kufikia sh. bilioni 294.
IGP Mwema alisema polisi imefanikiwa kuanzisha bodi yenye wajumbe tisa, ambapo Mwenyekiti ni Ali Mufuruki, huku wajumbe wengine wakiwa Yogesh Manek, Deo Mwanyika, Salum Bisarara, Paolo Chiaro, Nassor Salum, Mussa Ally Mussa, Suleiman Kova na Said Salim Bakhresa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru