Wednesday, 27 November 2013

Mauaji ya bodaboda yawatikisa Polisi Dar


Na Mohammed Issa
MATUKIO ya mauaji ya waendesha pikipiki maarufu kama Bodaboda na wengine kujihusisha kwenye uhalifu, yamezidi kushika kasi katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Tayari watu watatu wanadaiwa kupoteza maisha wilayani Ilala, Dar es Salaam, katika kipindi cha wiki moja baada ya kushambuliwa na makundi ya waendesha bodaboda kwa tuhuma za kupora pikipiki.
Kufuatia hali hiyo, Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, imetoa onyo kwa wanaojihusisha na matukio hayo, ikiwemo kujichukulia sheria mkononi na kusababisha mauaji.
Pia, imesema imeanza kukomesha matukio ya wizi wa pikipiki pamoja na mauaji ya wanaotuhumiwa kuiba pikipiki hizo.
Walisema kama kuna dereva au mmiliki wa pikipiki anapata usumbufu kwenye masuala ya kiupelelezi waonane na wakuu wa vituo ili kupatiwa ufumbuzi wa kesi zao.
Akizungumza na Uhuru kwa njia ya simu jana, Mkuu wa Upelelezi na Makosa ya Jinai, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Ahmed Msangi, aliwataka wamiliki na madereva wa boda boda kufuata sheria badala ya kujichukulia sheria mkononi.
Alisema kuanzia sasa, Polisi hawatavumilia vitendo vyovyote, vitakavyosababisha uvunjifu wa amani ikiwa ni pamoja na damu za watu kumwagika.
“Matukio ya wizi wa pikipiki yasiwe sababu ya watu kuuana, na si sahihi kumuua mtu kwa sababu hiyo, tunataka kila mmoja afuate sheria.
“Kama madereva wa bodaboda wanapata shida kwenye masuala ya upelelezi, waende kwa wakuu wa vituo au makamanda, kupatiwa ufumbuzi wa kesi zao…wasidhani kama wanapopeleka kesi hazifanyiwi kazi, wanapoona uzito waende mbele zaidi kuliko kujichukulia hatua,” alisema.
Kwa mujibu wa Msangi, Polisi wanajitahidi kudhibiti matukio ya wizi wa pikipiki na alitoa wito kwa jamii, kutoa ushirikiano ili kuwafichua wahalifu wa aina hiyo kwenye maeneo yao.
Alisema wananchi wajiepusha na uvunjifu wa sheria na kwamba, wanapomkamata mwizi, wampeleke kwenye vyombo vya sheria.
Msangi, alitoa kauli hiyo kufuatia ongezeko la mauji ya wanaotuhumiwa kuhusika na wizi wa pikipiki, kushamiri jijini Dar es Salaam.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Ilala, Marietha Minangi, alisema waendesha boda boda 16 wanashikiliwa na polisi kwa tuhuma za kufanya fujo na kusababisha mauaji ya mtu waliyedhani ni mwizi wa pikipiki.
Alisema kati ya watuhumiwa hao, mmoja alikamatwa na sare za Jeshi la Polisi.
Juzi, waendesha bodaboda zaidi ya 100, walifanya msako wa kuwasaka wezi wa pikipiki katika mtaa wa Kivule, Ilala Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Marietha, waendesha bodaboda hao, walimkamata mtu waliyedhani ni mwizi ambapo walimchukua mpaka Msongola na kisha walimpiga na kumchoma moto na kabla ya kufa papo hapo.
Alisema baada ya kufanya mauaji hayo, madereva hao, walikwenda Kivule CCM na kuvamia nyumba ya mtu waliyedhani ni mwizi wa pikipiki na kufanya uharibifu wa mali mbalimbali, ikiwemo magari mawili.
Kamanda huyo, alisema Polisi wanaendelea na msako wa kuwakamata waliohusika katika tukio hilo.
Alisema Polisi hawatakubali kuona vitendo vya mauaji ya raia vikiendelea kutokea, kuanzia sasa, wamejipanga kukabiliana na wanaotekeleza mauaji hayo.
Habari kutoka eneo la tukio, zilisema madereva wa bodaboda walijikusanya kwa ajili ya kufanya msako wa nyumba kwa nyumba baada ya kupata majina ya mtandao wa wezi wa pikipiki katika mtaa huo na maeneo ya jirani.
Yussuf Makame, ambaye ni dereva, alisema jana kuwa waliamua kufanya msako huo kufuatia vitendo vya wizi wa pikipiki kuendelea kushamiri katika maeneo hayo.
“Hapa tunalizwa sana, pikipiki nyingi zinaibiwa na kesi zikienda polisi zinachukua muda mrefu, ndio maana vijana wameamua kumalizana na wezi kwa kuwashambulia,” alisema.
Kwa mujibu wa Makame, licha ya kuibiwa bodaboda zao, baadhi yao wanauawa na majambazi hayo na kisha kutokomea sehemu zisizofahamika.
Alisema wanapowafikisha watuhumiwa hao polisi, upelelezi wa kesi huchukua muda mrefu na mara nyingine kesi zinamalizwa katika mazingira ya kutatanisha.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru