Wednesday 20 November 2013

Sumaye: Utatuzi wa masuala ya elimu ufanyike kwa haraka


NA MWANDISHI WETU
WAZIRI Mkuu  Mstaafu, Frederick Sumaye, tatizo la kushuka kwa kiwango cha ufaulu linapaswa kutatuliwa kwa haraka na kwamba kulumbana juu kubadilisha majina ya madaraja ya viwango vya ufaulu hakuna tija.

Sumaye alisema hayo jana katika mahafali ya 11 ya shule ya Sekondari ya wasichana ya Amani inamilikiwa na Shirika la Masista Waabuduo Damu ya Kristo, Jimbo Katoliki la Singida.
ìLeo tunaanza kulumbana kama matokeo ya kidato cha nne yawe na daraja sifuri au daraja hilo sasa liitwe daraja la tano na kwa kufanya hivyo kiwango cha kufeli sasa kianzie alama 20 badala ya 34 ya huko nyuma.
ìUtafiti unaonyesha hata kiwango cha ufaulu wa alama 34 yenyewe iko chini sana, je tukikishusha kiwango hicho itakuwaje? Kama badiliko hili litapitishwa, basi itaingiza sura mpya kabisa katika shule zetu,î alisema.
Alisema hakuna mtihani usio na madaraja na daraja la mwisho ni la walioshindwa kufikia kiwango cha kufaulu.
Unapokuwa na daraja F au 0, si kwamba huna chochote kichwani, bali kilichoko hakifikii kiwango kinachotakiwa kwa kufaulu,î alisema Sumaye.
Alisema kama isivyo sahihi kwa mwanafunzi aliyepata alama 34 kupewa daraja 0, hata aliyepata alama 5 naye hastahili kupewa daraja 0 maana na yeye ana kitu japo kidogo kichwani.
Hata hivyo, aliipongeza Kamati ya Kudumu ya Huduma za Jamii ya Bunge kwa kuona upungufu huo na kuishauri serikali kipi cha kufanya.
ìNi matumaini yangu kuwa serikali yetu sikivu itauchukua ushauri huo kwa umuhimu unaostahili,î alisema Sumaye.
Alisema dawa ya matatizo haya yanayojitokeza sasa katika sekta ya elimu ni kuboresha mazingira ya utoaji wa elimu na si kucheza na mitaala au kushusha alama za ufaulu.
Sumaye  pia alionya  wanaoiangalia elimu katika sura ya kupata ajira ya ofisini  kuwa si fikra sahihi na mawazo hayo hayapaswi kuendekezwa.
Huku akinukuu vifungu vya Biblia na nukuu za Baba wa Taifa Julius Nyerere, Sumaye alisema; ìKatika kitabu kitakatifu cha Biblia, tunaambiwa ëMkamate sana elimu, usimwache aende zake; Mshike, maana yeye ni uzima wako. Mithali 4:13.î
Alisema katika kitabu cha Elimu ya Kujitegemea, hayati Mwalimu Nyerere, aliandika kuwa lengo la elimu ni kurithisha kutoka kizazi kimoja hadi kingine maarifa na mila za taifa, kulitumikia na kuliendeleza Taifa.
Mwalimu Nyerere alifafanua kuwa lengo la elimu ya sekondari ni kuwapatia vijana elimu, ufundi na fikra ambazo zitawafaa wakati watakapoishi katika jamii inayobadilika,î alisema Sumaye.
Hivyo, alisema maana ya elimu si kuwapatia ajira pekee vijana wamalizao masomo yao, bali ilenga kuwawezesha kujiajiri ili wamudu maisha yao na kuwapatia fikra mpya zinazokwenda na wakati.
ìHivyo ni dhahiri kuwa yeyote anayepata fursa ya kusoma, anakuwa na bahati, maana amepata uhai, anapata ufunguo wa maisha bora na anakuwa na bahati ya kuutumikia umma walau kurudisha asante au fadhila kwa yote ambayo jamii imemsaidia mpaka akapata elimu,î alisema.
Alisema ajira itaendelea kuwepo na watakao ajiriwa ni wale watakao kuwa na  elimu nzuri.
Hivyo, alitoa rai kwa wazazi na walezi nchini, kuwahimiza watoto wao wasome kwa bidii ili wawe washindani wazuri katika soko finyu la ajira.
Alitolea mfano elimu ya sayansi na teknologia, kuwa itaendelea kuwa na soko kubwa kwa muda mrefu katika ulimwengu wa utandawazi kutokana na mahitaji yake.
ìNi kweli ajira katika soko rasmi haikui kwa kiwango sawa na idadi ya wanaohitaji ajira katika soko hilo, lakini hii si kwa Tanzania tu, bali ni kwa nchi zote duniani.
ìHivyo tusitarajie kuwa kuna siku itafika vijana wote wanaomaliza kidato cha nne, cha sita na vyuo vya elimu juu tutawakuta wote maofisini wamevaa tai wameajiriwa na soko rasmi, si kweli,î alisema Sumaye.
Alisema umefika wakati sasa wa kuichochea sekta isiyo rasmi ikue kwa kasi, ili kila Mtanzania apate fursa ya kujiajiri.
ìHapa ndipo elimu itawawezesha watu wamudu ushindani hata katika sekta hiyo pia,î alisisitiza.
Akizungumzia malumbano yaliyoibuka hivi karibuni kuhusiana na viwango vya madaraja ya ufaulu, alisema tangu kale elimu ilipewa nafasi ya pekee katika maisha ya binadamu, tofauti kubwa ilijionyesha kati ya watu wenye elimu na ambao hawakuwa nayo.
ìHali kadhalika hata katika ulimwengu wa leo, elimu bado imeendelea na itaendelea kutoa tofauti kati ya wenye elimu na wasio na elimu au hata kati ya wenye elimu bora na wasio na elimu bora,î alisema Sumaye.
Alisema nchi zilizozingatia utoaji wa elimu bora, zimeendelea kufanya vizuri katika medani za maendeleo, ikilinganishwa na ambazo hazikuzingatia.
ìMaendeleo ya haraka ya viwanda na teknolojia katika nchi mbali mbali duniani yametokana na nchi husika kuzingatia utoaji wa elimu katika fani za sayansi na teknolojia kwa watu wao hasa vijana,î alisema Sumaye.
Alisema ili kufikia malengo, nchi inapaswa kutoa elimu bora kwa watoto na vijana kwa lengo la kuondoa ujinga ambao ni chanzo cha matatizo mengi katika jamii, yakiwemo ya  umasikini na maradhi.
Sumaye alisema ifike wakati sasa Watanzania wajengewe imani kwa vitendo, kuwa elimu inayotolewa na taasisi na shule nchini, iwe na ubora usiotiliwa shaka na mtu yeyote. Alisema haitakuwa busara kwa taifa kusomesha watoto wote, lakini kwa viwango vya chini kuliko vinavyokubalika.
ìLazima elimu yetu iwe na ubora kitaifa kulingana na mitaala inayokubalika, na pia iwe na ubora wa kimataifa.
ìTusijitengenezee viwango vyetu wenyewe ambavyo havikubaliki au vinatiliwa shaka na watu wengine au hata sisi wenyewe,î alionya Sumaye.
Hivi karibuni  Naibu Waziri wa Elimu,  Philipo Mulugo alitofautiana na Katibu Mkuu wa Wizara  hiyo, Profesa Sifuni Mchome juu ya viwango vya alama za ufaulu na ubadilishaji wa madaraja , suala ambalo limezua mjadala mkali ambapo mpaka sasa bado haujalewa masimamo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru