Friday 8 November 2013

Muswada wa magazeti wakataliwa

NA STEPHEN BALIGEYA, DODOMA
BUNGE limeondoa kifungu cha nane cha sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali ya mwaka 2013, iliyowasilishwa na serikali mapema wiki hii.
Akiwasilisha muswada huo Jumatano, wiki hii  mjini Dodoma, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema, alisema muswada huo  unapendekeza katika Ibara za 40 na 41 kuwa vifungu hivyo virekebishwe kwa lengo la kuongeza adhabu ya faini kwa makosa ya lugha na kauli za uchochezi katika magazeti, adhabu isiyozidi sh. milioni tano.
“Marekebisho haya  katika sheria ya magazeti (Sura 229) yanalenga kutekeleza Azimio la Bunge katika mkutano wa 11, kikao cha 21, ambapo Bunge liliazimia, pamoja na mambo mengine, kwamba serikali ipitie sheria zilizopo ili kuona kama  zinatosheleza kuzuia lugha au kauli za uchochezi,”alishauri Werema.
Alisema serikali imepitia sheria ya magazeti na kuona kuwa inazuia uchapishaji wa habari zinazoweza kusababisha uchochezi au uvunjifu wa amani kama inavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani chini ya vifungu hivyo ni sh. 150,000.
Jaji Werema alisema adhabu hiyo ni ndogo kulinganisha na madhara ya kosa husika katika jami, na ndiyo maana imependekezwa adhabu isiyopungua sh. milioni tano.
Hata hivyo, wakati wabunge wakichangia kwa kupinga kifungo hicho cha muswada cha Ibara za 39, 40, na 41, Werema aliwaeleza kama wataamua kuondoa kifungo hicho wafanye hivyo ila yeye hataweza kukiondoa kwa kuwa kazi yake ni kuhakikisha waovu wanadhibitiwa.

Akichangia muswada huo, Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Peter Selukamba, alisema hapingani na sheria iliyowasilishwa na serikali juu ya kuongezwa kwa adhabu kwa waandishi wanaokiuka maaadili, lakini lazima serikali itambue kuwa sheria hiyo ya magazeti ya mwaka 1976 imepitwa na wakati.
“Wakati nachangia juzi muswada huu, nilipendekeza kifungu chote cha nane kiondolewa mpaka pale tutakapoleta sheria ya magazeti, ili kuwatendea haki, maana huwezi kuwa na adhabu bila kuwapatia haki zingine,”alieleza Serukamba.
Alisema suala la kunyofoa sehemu tu ya Sheria ya Vyombo vya Habari na kuileta bungeni ili ipitishwe ni dalili kuwa kuna jambo ambalo lina manufaa kwa watu wachache.
‘’Tulete sheria nzima ya vyombo vya habari si kunyofoanyofoa sehemu tu na kuileta hapa hiyo itakuwa kuna sababu kwanini iwe hivyo,”alisema Serukamba.
Alisema ni muhimu wakati wa kuzungumzia adhabu hizo, kuangalia jinsi ya utendaji wa kazi wa waandishi wa habari kwani pia nao wana malalamiko mbalimbali ikiwemo viwango duni vya mishahara na mazingira ya utendaji wa kazi.
Serukamba alisema kama ni kauli za uchochezi basi zingine hutolewa na wanasiasa wenyewe kwani ndio wanowatumia, hivyo ni muhimu kutoa sheria itakayowatendea haki.
Hoja ya Serukamba iliungwa mkono na Mbunge wa Peramiho (CCM), Jenister Mhagama, ambaye alitaka kupelekwa kwa muswada wa sheria ya vyombo vya habari kwa kuwa tayari kamati ilishasema kuwa iko tayari, hivyo haoni sababu ya serikali kuona kigugumizi kupeleka sheria hiyo.
Akitoa ufafanuzi wa hoja hiyo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana  na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, alisema muswada huo uko tayari ingawa kuna marekebisho ambayo yanafanyiwa kazi kabla ya kupelekwa bungeni.
“Sidhani kama marekebisho haya wanaweza kushindwa kupitishwa kwa sababu ya kutokuja kwa muswada huo wa sheria ya magazeti,”alieleza Dk. Mukangara.
Akitoa ufafanuzi wa hoja hiyo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alisema kuwa  katika eneo  ambalo serikali imefanyia utani ni katika sheria hiyo, hivyo kuwataka kuipeleka bungeni.
“Tumewaagiza mara nyingi mlete, lakini hamfanyi, lazima mjue tuko makini kuhusu sheria ya magazeti mkoa pole pole mno bila sababu za msingi, tukitunga sheria ya magazeti tutakuwa salama zaidi,”alieleza Spika Anne.
Katika kutaka kuhakikisha hoja hiyo, haiondolewe baada ya wabunge wengi kuunga mkono ya kuondoa kwa kifungu hicho chote cha nane, Werema alitaka bunge lipige kura kwa kuita majina ya wabunge, jambo ambalo lilikataliwa na Spika na kukifanya bunge kukiondoa.
Wakichangia  katika muswada huo, wabunge mbalimbali walipinga kifungu hicho, ingawa kuna baadhi waliotaka kisiondolewa ili kudhibiti nidhamu ya waandishi wanaotumiwa.
Mbunge wa Mbozi Mashariki (CCM), Godfrey Zambi, alisema ni muhimu kwa waandishi wa habari kuwa wazalendo na nchi yao na kutetea taifa lao katika uandishi wao.
Zambi alisema pamoja na kuweka sheria hiyo, lazima kuweka sheria kali dhidi ya lugha za uchochezi zinazoandikwa katika baadhi ya vyombo vya habari.
‘’Bado kuna umuhimu kwa serikali kuweka adhabu juu ya masuala ya kuandika habari za uchochezi na kama wapo watu wanaona kuwa kuweka adhabu hizo ni kuwanyima haki waandishi, basi hao wanataka kuvitumia vibaya vyombo hivyo kwa maslahi yao,”alieleza.
Katika hatua nyingine, bunge limepitisha muswada wa marekebisho ya sheria mbalimbali pamoja na baadhi ya marekebisho yaliyofanywa na wabunge.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru