Tuesday 19 November 2013

Ajira za vigogo wa KIA zawekwa rehani


NA SHAABAN MDOE, ARUSHA
AJIRA za vigogo wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), zimewekwa rehani.
Hatua hiyo inatokana na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, kusema atawafukuza kazi pindi atakapata taarifa ya kupita kwa wahamiaji haramu, dawa ya kulevya na nyara za serikali.
Dk. Mwakyembe alitangaza kiama hicho na kuweka rehani ajira hizo jana, alipozungumza na menejimenti na watumishi wa Kampuni ya Uwakala katika uwanja huo ya KADCO ili kujua uendeshaji na changamoto zinazowakabili.

Alisema ana taarifa za kutosha kuhusu baadhi ya wafanyakazi wa kampuni hiyo, hasa Kitengo cha Usalama na Uhamiaji wanaoshiriki kutoa hati feki za kusafiria, kuvusha dawa za kulevya na nyara za serikali, jambo ambalo hatalivumilia kwa kuwa linaitia doa nchi, kimataifa.
Mwakyembe alisema vitendo hivyo vimeshamiri kwa kasi katika uwanja huo kipindi kifupi baada ya kudhibiti vitendo hivyo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere (JNIA) Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa waziri huyo, baadhi ya watu ambao wanajihusisha na biashara hizo haramu, wameugeuza uwanja huo kuwa uchochoro.
Alisema atahakikisha kila aliyehusika katika utekelezaji wa matendo hayo maovu anatimuliwa, hata kama yuko wizara tofauti na anayoiendesha kwa kuwa wafanyakazi wote wanafanya kazi chini ya serikali moja inayoongozwa na Rais Jakaya Kikwete.
Waziri Mwakyembe alisema kuanzia sasa atazungumza na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, kuhusu jambo hilo na kumtahadharisha kuwa atamshangaa pindi atakapompokea mtumishi wa wizara yake ambaye atabainika kuhusika na masuala hayo.
ìHapa hakuna cha kwamba mimi niko Wizara ya Mambo ya Ndani, kwamba huhusiki... mimi na nyinyi sote tuko chini ya serikali moja, na nitampigia simu Waziri Nchimbi nimwambie kuwa nitamshangaa endapo atampokea mtumishi nitakayemfukuza kazi kwenye wizara yangu,î alisisitiza Dk. Mwakyembe.
Hata hivyo, aliutahadharisha uongozi wa KADCO kuanza kuwachukulia hatua kali za kisheria watumishi wanaoonekana kushiriki vitendo hivyo viovu, hususan usafirishaji wa dawa za kulevya, nyara za serikali na utoaji wa hati feki za kusafiria, vinginevyo akiligundua yeye kosa hilo na wao kuwa kimya, hawatasalimika.
Alisema mtu yeyote atakayekamatwa akiwa na hati feki ya kusafiria, nyara za serikali na dawa za kulevya na kubainika alipitia KIA, uongozi mzima na wale waliokuwa zamu watawajibika kutafuta kazi nyingine ya kufanya.
ìMuda umekwisha naomba anzeni kuwataja wale wote wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya, meno ya tembo na hati feki, na msingoje nije hapa nyie mkisikia tu naulizia jambo hilo, bakini nyumbani mtafute kazi za kufanya. Barua zenu mtaletewa kwenu ili mjisafishe badala ya kuendelea kuchafua jina zuri la uwanja huu,î alisema Dk. Mwakyembe.
Akijibu hotuba ya Mwenyekiti wa Bodi ya KADCO, Balozi Gumbo Kibelloh, Waziri Mwakyembe, alipongeza mafanikio yaliyofikiwa na uwanja huo ya kuongeza idadi ya ndege, tuzo mbili kubwa za kimataifa zilizopatikana kutokana na kazi nzuri iliyofanyika.
Alisema kiwango cha ongezeko la asilimia 25 kwa jumla kwa wageni wa kimataifa kutoka asilimia 12 na wale wa ndani kufikia asilimia 36 na asilimia 44 kwa wanaobadilisha ndege ni suala la kujivunia, kwani ni mafanikio makubwa kwa uwanja huo hadi kuwa uwanja wa pili kwa ubora baada ya Australia.
Nakumbuka Novemba 12 au 13, nilipokea simu ya mwekezaji akiwa na ndege ya KLM, ambapo walifika hapa na kukuta giza tupu baada ya umeme kukatika. Sasa hii ni aibu kubwa na inaweza kutupunguzia mashirika makubwa ya ndege ya kimataifa, lakini niliongea na TANESCO wanalishughulikia hilo,î alisema Dk. Mwakyembe.
Katika taarifa yake, Balozi Kibelloh alisema KIA unaliingizia taifa fedha nyingi kupitia kiwango kikubwa cha kodi ya zaidi ya sh. bilioni moja inayolipwa na uwanja huo kutokana na shughuli mbalimbali.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru