Thursday, 14 November 2013

Asilimia tisa ya Watanzania wanaugua kisukari


NA RACHEL KYALA
TAKWIMU zinaonyesha kuwa asilimia 9.1 ya Watanzania wenye umri wa miaka 25 na kuendelea wana ugonjwa wa kisukari.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Hussein Mwinyi, aliyasema hayo jana alipokuwa akitoa tamko la maadhimisho ya siku ya kisukari duniani ambayo huadhimishwa Novemba 14, kila mwaka.
Aidha, Dk. Mwinyi alisema takwimu hizo ni za utafiti uliofanyika mwaka 2012 ambazo zilihusisha takriban wilaya 50 kote nchini, ambapo Tanzania inashika nafasi ya nane miongoni mwa nchi 10 zinazoongoza kwa kisukari barani Afrika.
“Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu inasema ‘linda maisha yajayo dhidi ya ugonjwa wa kisukari’ ambayo inalenga kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu kinga na mambo yanayoongeza uwezekano wa kupata maradhi yasiyo ya kuambukiza ikiwemo kisukari,” alisema.
Dk. Mwinyi aliyataja magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza kuwa pamoja na kisukari, magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, saratani na magonjwa sugu ya njia ya hewa.
Pia, alieleza mambo yanayoongeza uwezekano wa kupata magonjwa hayo kuwa pamoja na ulaji uliokithiri, matumizi ya chumvi kwa wingi, mafuta na sukari, uzito uliozidi, unene uliokithiri, kutofanya mazoezi, ikiwemo uvutaji wa sigara na bidhaa zitokanazo natumbaku.
Aliongeza kuwa mambo mengine ni unywaji pombe kupita kiasi na msongo wa mawazo.
Alisema serikali inaendelea kuandaa miongozo na mikakati ya kisera kwa kushirikisha jamii katika kudhibiti magonjwa yasiyo ya kuambukiza, ikiwemo kuungana na mataifa maengine duniani kuhakikisha kuwa inayapunguza kwa asilimia 25 ifikapo 2015.
Waziri Mwinyi alizitaja dalili za ugonjwa wa kisukari kuwa pamoja na kiu isiyoisha, kukojoa mara kwa mara, kupungua uzito, kusikia njaa kila wakati, ikiwemo mwili kukosa nguvu.
“Nawashauri wananchi kupima afya ili kubaini kama wana kisukari, kwani mtu anaweza kukaa muda mrefu na ugonjwa huu pasipo bila kuwa na dalili yoyote, ambapo kadri sukari inavyopanda inaharibu mishipa ya fahamu na damu, figo kushindwa kufanya kazi, macho na kusababisha upofu, moyo, miguu kufa ganzi na kuwa na vidonda,” alisema.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru