Tuesday, 19 November 2013

Wanaotambiana CCM wazodolewa


NA SULEIMAN JONGO, SONGEA
KATIBU Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, amesema viongozi wanaotambiana, kupigana vikumbo na kusema hadharani kupitia vyombo vya habari hawana sifa ya kuwa viongozi bora.
Amesema wanaofanya hivyo wanasukumwa na ulafi wa mali na uroho wa madaraka. “Wameshindwa kutumia muda wao kushughulikia matatizo ya wananchi, badala yake wanapigana vikumbo kusemana na kushambuliana kwa lengo la kupata uongozi.”
Kinana aliyasema hayo jana, mjini Peramiho wilayani hapa mkoani Ruvuma, alipozungumza na wajumbe wa shina namba 26 lililoko katika Kata ya Peramiho.
Aliwataka wana-CCM kutowachagua viongozi wa aina hiyo kwenye nafasi za uongozi kwa kuwa, dhamira yao si kuwatumikia Watanzania, bali wanataka kujilimbikizia mali.
"Wote walioko juu wanaosemana kupitia vyombo vya habari hawafai. Kusemana kwao kunawaondolea heshima, hivyo wazomeeni hao kwa kuwa si viongozi bora, hawana heshima na sifa stahili,î alisema.
Kinana alisema wanaoshindana na kurushiana maneno wanalipwa fedha, posho na wengine mishahara ambayo huwapa shibe na kuwahamasisha kuwa na uroho wa madaraka.
Alifafanua kuwa, ili kuamini kauli hiyo siku zote wanaosemana ni viongozi wa juu, na kwamba katu huwezi kusikia mabalozi wa nyumba 10 na wanachama wa kawaida wakijibizana au kusuguana kupitia vyombo vya habari.
ìHivi mmewahi kusikia wapi mabalozi wa nyumba 10 wanagombana na kushambuliana kwenye magazeti. Haiwezi kuwa hivyo kwa sababu hakuna wanacholipwa, bali kazi yao ni kuwatumikia wananchi na CCM,” alisema Kinana.
Alisema wananchi wanataka kutatuliwa kero na changamoto zinazowakabili na si malumbano, kwani wanaofanya hivyo wanafanya kwa sababu ya madaraka, wanaleta aibu.
Hii ni aibu, aibu, aibu tena aibu kubwa, viongozi kusema kwenye vyombo vya habari kisa madaraka ni aibu.
Katibu Mkuu aliongeza kuwa viongozi wa aina hiyo ndio wanaokivuruga Chama badala ya kutoa ushirikiano kutatua matatizo ya wananchi.
Awali, akimkaribisha Kinana katika eneo hilo, Kiongozi wa Kimila na Mwenyekiti wa CCM Tawi la Maposeni, Julius Ndiu, alimkabidhi silaha za jadi ambazo ni ngao, mgolole, mkuki na shoka dogo ni silaha anazotakiwa kuzitumia katika kukilinda Chama.
ìNakukabidhi silaha hizi kwa ajili ya kupambana na mafisadi ndani ya Chama na kuwapiga vita wanaokwamisha maendeleo ya CCM,” alisema.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru