na mwandishi wetu
WANANCHI wa kada mbalimbali, wakiwemo wasomi nchini, wamewashukia baadhi ya wabunge wa CCM, wakisema ni wasaliti na wanakwenda kinyume na malengo ya Chama na serikali.
Pia, wamekishauri Chama kuwa umefika wakati wa kuwachukulia hatua kali viongozi wake, wakiwemo mawaziri na wabunge, ambao watabainika kwenda kinyume na dhamira yake katika kuwatumikia Watanzania.
Kauli hizo zilitolewa kwa nyakati tofauti kutokana na mambo yanavyoendelea ndani ya Bunge, ikiwemo hoja mbalimbali za wabunge zinazowasilishwa, ambazo zingine zinadaiwa kuwa na sura ya maslahi binafsi zaidi.
Waliyasema hayo jana wakati wakizungumza na Uhuru, kutoa maoni kuhusu mwenendo wa Bunge na mustakabali wa rasilimali za taifa, wakiwemo wanyama, ambao wako kwenye hatari ya kutoweka kwa sasa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mzumbe, Mohamed Bakari, alisema tatizo la uwajibikaji kwa baadhi ya viongozi ndiyo inayolifanya taifa lishindwe kufikia malengo.
Alisema baadhi ya viongozi ndani ya Bunge na Baraza la Mawaziri, wameshindwa kuwajibika kikamilifu, hivyo wamebaki kuwa watengeneza mizengwe dhidi ya wengine, ambao wameamua kulitumikia taifa.
Pia, alieleza kushangazwa na hatua ya baadhi ya wabunge kuungana kupinga Operesheni Tokomeza, ambayo ilikuwa na lengo zuri la kulinda rasilimali za taifa kutokana na kushamiri kwa wimbi la majangili.
Alisema operesheni hiyo imekuwa na mafanikio mazuri, na kwamba ambao ilipaswa kuendelezwa, lakini baadhi wameamua kuipinga.
ìWapo waliopinga operesheni hii ya kudhibiti ujangili, hapa inawezekana kuna baadhi ya viongozi wanahusika na biashara ya nyara za taifa, hivyo ikiendelea mambo yao yatakwama, jambo ambalo ni hatari,î alisema Bakari.
Kutokana na hilo, amesema ni vema CCM ambayo ndio imeshika dola ikafanya maamuzi magumu ya kuwaondoa viongozi wote wasaliti na wanaokwenda kinyume na dhamira ya Chama.
Pia, alisema changamoto nyingine za kimtazamo kuhusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, jambo ambalo limewafanya baadhi ya viongozi kushindwa kushirikiana katika utekelezaji wa majukumu, hivyo kurudisha nyuma maendeleo.
Naye Mkuu wa Idara ya Sayansi na Utawala wa Umma katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Benson Bana, alisema hakurajia kama wabunge wangefanya maamuzi ya kupinga Operesheni Tokomeza, kwani lengo lake lilikuwa zuri.
Alisema wabunge walitakiwa kuwa mstari wa mbele kuunga mkono jitihada za serikali, ikiwa ni pamoja na kujitokeza kushiriki kwenye maeneo yao.
ìKitendo cha kupinga kinawafanya watu wahoji uzalendo wa wabunge wetu kwa sababu hakuna asiyefahamu madhara ya ujangili. Kupinga ni sawa na kuhujumu uchumi, jambo ambalo ni fedheha,î alisema.
Dk. Bana alisema operesheni hiyo ilikuwa nzuri na ilikuwa na mustakabali wa kulinda maslahi ya taifa, hivyo hakukuwa na sababu ya kubeza jitihaza hizo.
ìKama ningekuwa nachunguza kuhusu biashara hii, ningeanza kuangalia mienendo ya wabunge wote waliopinga na maslahi waliyonayo katika biashara hii, kimsingi maslahi ya taifa yanatakiwa yalindwe kwa gharama yeyote.
ìUmefika wakati wabunge wajielekeze katika kusimamia mambo ya msingi na yenye kulinda maslahi ya taifa, hakuna jambo zuri lisilokuwa na madhara na changamoto zilizojitokeza katika operesheni hiyo zilitakiwa kutatuliwa na mambo yakaendelea na si kuisitisha wakati tembo wanazidi kuuawa kila kukicha,î alisema.
Naye Johnson Mwakijambili, alisema viongozi wanapaswa kuacha unafiki mbele ya wananchi na badala yake wawajibike ili nchi isonge mbele.
Pia, alishangazwa na hatua ya baadhi ya mawaziri kushindwa kuitetea Operesheni Tokomeza, ambayo ilipewa baraka katika vikao halali.
“Mawaziri wahudhurie vikao ili wasikilize hoja badala ya kutoroka, ndio haya mambo yanayofanya washindwe kutetea hoja na shughuli wanazokubaliana bungeni,” alisema.
Tuesday, 5 November 2013
Wabunge CCM ni wasaliti -Wasomi
08:29
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru