Wednesday, 20 November 2013

TCAA yawakana marubani


Na Mwandishi Wetu
MAMLAKA ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), imesema haihusiki na malalamiko ya marubani wa Kitanzania kukosa ajira katika mashirika ya ndege, licha ya kuwa na leseni zilizotolewa na mamlaka.
Pia, TCAA imesema mamlaka hiyo ipo kuangalia maslahi ya pande zote na sio mdau mmoja, hivyo ni wakati wa chama cha marubani kuthamini mchango wa mamlaka hiyo na si kuivunja nguvu.
Msimamo wa TCAA ulitolewa jana katika taarifa iliyotumwa kwenye vyombo vya habari, kuhusiana na malalamiko ya chama cha marubani kuhusiana na matatizo wanayokumbana nayo.
Taarifa hiyo ilisema mamlaka haihusiki na matatizo ya marubani hao, kwani haikushiriki katika mchakato wa wao kwenda mafunzoni na hakuna mkataba wa kuwaendeleza, kwani kazi ya mamlaka ni udhibiti wa sekta (masuala ya ki-usalama  na kiuchumi) na sio kutoa mafunzo au ajira kwa kuwa haina ndege.
Ilisema katika miezi ya hivi karibuni, kumekuwepo na taarifa za malalamiko ya baadhi ya marubani wa Kitanzania kuhusu kukosa ajira katika mashirika ya ndege yanayoendesha shughuli zake hapa nchini, licha ya kuwa na leseni zilizotolewa na TCAA zinazothibitisha kuwa wamefuzu kufanya kazi hizo za urubani.
Katika malalamiko hayo,  marubani kupitia chama chao, wameinyooshea kidole TCAA kuwa imeshindwa kutatua tatizo hilo na kwamba imeonekana kuegemea upande wa watoa huduma za usafiri wa anga nchini, ambao chama kinawatuhumu kutoa ajira kwa upendeleo.
Aidha, taarifa ilisema chama hicho kiliituhumu TCAA kuwa ilipuuza ushauri wake uliotaka kipaumbele cha udhamini wa mafunzo ya urubani kupitia Mfuko wa Mafunzo ya Marubani na Wahandisi Ndege kutolewa kwa marubani Watanzania ambao hawajapata ajira ili kuwajengea uwezo na hivyo kuwaongezea sifa za kupata ajira, na kuichukulia mamlaka kama kikwazo cha jitihada zao katika kupata ajira.
Taarifa ya TCCA ilisema matatizo mengi yanatokana na mabadiliko katika sekta, ambapo awali marubani kama ilivyokuwa katika fani nyingine, waligharimiwa mafunzo yao na serikali au wafadhili, ikiwemo mafunzo ya marubani yaligharimiwa na Shirika la Ndege Tanzania (ATC) na Wakala wa Ndege za Serikali.
Ilisema kuanzia miaka ya 1980, mfumo wa mafunzo ulibadilika ambapo wanafunzi kupitia wazazi au walezi wao wamekuwa wakijigharimia mafunzo yao wenyewe. Licha ya kufanikiwa kufanya mafunzo ya awali, inakuwa vigumu kwa watu binafsi kulipia gharama kubwa za mafunzo zaidi.
Hivyo, taarifa ilisema chama cha marubani kinaelewa kuwa juhudi za mamlaka kushawishi serikali na wenye ndege waweze kusaidia kupunguza tatizo la ajira, hatua hizo zimeanza kuzaa matunda, hivyo wauthamini mchango wa mamlaka na sio kuivunja nguvu.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru