Wednesday 20 November 2013

Mwakyembe ashtukia janja ya mwekezaji


NA SHAABAN MDOE, ARUSHA
SAKATA la kudaiwa kuuzwa kwa kipande cha eneo la reli kwa mwekezaji Arusha limechukua sura mpya baada ya Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, kuonyesha wasiwasi  juu ya taarifa za kukodishiwa eneo hilo kwa miaka miwili huku mwekezaji akitumia sh. milioni 500 kujenga uzio.
Dk. Mwakyembe akizungumza katika eneo hilo alisema taarifa kuwa mwekezaji huyo, Philimon Mollel, kupitia Kampuni ya Monaban,  ambaye amepewa eneo hilo na Shirika Hodhi la Kusimami Mali za Reli (RAHACO) kwa miaka miwili  kwa ajili ya maegesho ya magari yake, alisema litakuwa na undani zaidi kwa kuwa hakuna anayeweza kutumia fedha nyingi kiasi hicho kujenga ukuta kwa ajili ya maegesho ya magari kwa miaka miwili tu.
Kabla ya Dk. Mwakyembe hajatoa maamuzi kuhusu suala hilo, alimpa nafasi Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema,  kuzungumza ambapo alisema anachokiamini ni kwamba mwekezaji huyo ana lengo la kulitwaa eneo hilo kiujanja ambapo kwa sasa ameonyesha kulihitaji tu kwa ajili ya maegesho ya magari na kuwa hiyo sio nia yake pekee.
ìMheshimiwa Waziri hapa ninachokiona ni mpira umetangulizwa mbele halafu anapima upepo, tukinyamaza sisi pamoja na nyie serikali, kesho mtakuta mambo mengine yanafanyika hapa....mimi nakueleza wazi usikubali kudanganywa,îalisema Lema.
Mbunge huyo aliongeza kuwa hivi karibuni katika kikao cha Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi inayongozwa na Dk. Hamis Kigwangwala ilipokuwa Arusha, ilimuita na kumuhoji mwekezaji huyo ambaye alikuwa na majibu tofauti tofauti juu ya matumizi ya baadaye ya eneo hilo.
Alisema mara ya kwanza aliieleza kamati hiyo kuwa aliliomba eneo hilo na kupewa kwa mkataba wa miaka miwili kwa ajili ya kufanya shughuli za maegesho na kuoshea magari yake na magari ya wananchi wengine kama njia ya kutoa ajira kwa vijana wapato 150.
Lema alisema kutokana na maelezo yake hayo,  kamati ilimhoji iwapo kuna mwekezaji anaweza kutumia sh. milioni 500 kujenga ukuta kwa ajili ya kuegesha magari kwa mkataba wa miaka miwili kwa kuwa itakua ni sawa na kutupa fedha zake au vinginevyo ana lengo lingine tofauti ya kulitwaa kinyemela eneo hilo.
Aliongeza kuwa baada ya kuulizwa swali hilo, mwekezaji huyo alijibu kuwa siyo fedha zote sh. milioni 500 amezitoa yeye,  bali wamegawana nusu kwa nusu na wamiliki wa eneo hilo RAHACO kwa niaba ya Shirika la Reli  Tanzania (TRC) ambapo yeye alitoa sh. milioni 250.
Lema alisema mara baada ya mwekezaji huyo kuona amebanwa juu ya suala hilo, alitoa maelezo ya nyongeza kuwa mbali na uwekezaji huo wa maegesho na kuoshea magari,  ana mpango wa kujenga majengo ya kibiashara na stesheni ya treni.
Mbunge huyo alisema kutokana na maelezo hayo, pamoja na kamati nzima waliingiwa na wasiwasi juu ya uwekezaji huo wa sh. milioni 500 ukilinganisha na faida anayoipata kutokana na maegesho ya magari yake binafsi na eneo la kuoshea magari yake na ya wananchi wengine.
Kutokana na mkanganyiko huo, Lema alimshauri Waziri Dk. Mwakyembe kuwa eneo hilo iwapo lingetangaziwa zabuni ya kukodishwa na TRC wenyewe kupitia wasimamizi wake RAHCO, serikali ingeweza kupata fedha nyingi kiasi cha sh. milioni 15 kwa mwaka tofauti na fedha wanayolipwa sasa ya sh. 500,000 kwa mwezi.
Kutokana na maelezo hayo, Dk. Mwakyembe alimuuliza mwekezaji huyo iwapo ni kweli ana nia ya kujenga maduka hayo na stesheni ya reli na njia zake baada ya kukabidhiwa eneo hilo kwa mkataba wa miaka miwili ya uwekezaji mdogo na wa muda mfupi.
Mwekezaji huyo alimjibu kuwa ni kweli na tayari ameshafanya mawasiliano ya namna ya kupata vichwa viwili vya treni na mabehewa kutoka Afrika Kusini, jambo ambalo lilimashangaza waziri.
Hapo hapo, aliwageukia viongozi wa RAHCO na kuwahoji aliyewapa ruhusa ya kufanya makubaliano ya namna hiyo bila kuishirikisha ofisi yake ambapo walijibu kuwa hakuna makubaliano ya namna hiyo baina yao na mwekezaji huyo katika mkataba wao.
ìKumbe kuna mambo makubwa hivyo, sasa nikwambie Mollel kama kuna kitu nyuma ya pazia mbali na haya tunayoelezwa hapa katika mkataba wenu, tambua hakitafanyika, hakuna kujengwa kwa ‘shopping mall’ wala stesheni ya treni na njia zake. Hiyo ni kazi ya wizara,”alisema Dk. Mwakyembe.
Alimtaka mwekezaji huyo kuendelea na shughuli zake za uegeshaji wa magari yake pamoja na uoshaji magari katika eneo hilo kama mkataba unavyosema pasipo kuongeza ujenzi wa jengo lolote la kudumu kwa kuwa siku yoyote baada ya mkataba wake wa miaka miwili kumalizika serikali italichukua eneo hilo kwa ufufuaji wa njia za reli.
ìNdugu yangu endelea na kazi zako kwa mujibu wa mkataba wako na hawa jamaa baada ya hapo tuna mpango wa ujenzi wa reli kutoka Tanga hadi Musoma, hivyo usijidanganye kufanya ujenzi mwingine kwa kuwa hutafanikiwa. Sitaki kusikia siku tunataka eneo letu uanze kuleta habari zako za mahakamani, kwa kuwa hutashinda,îalisema Dk. Mwakyembe.
Katika habari ya mwanzo iliyoandikwa na gazeti dada na hili la MZALENDO, Mkurugenzi Mtendaji wa RAHCO, Mhandisi Tito, alikiri kutoa kibali kwa mwekezaji kwa ajili ya ujenzi wa uzio huo hadi kuingilia eneo la barabara ya treni kwa maelezo kuwa maamuzi hayo yalifikiwa na bodi nzima ya RAHCO.
Gazeti hili pia lilimnukuu Mkurugenzi wa Kampuni ya Monaban Mollel ambaye alisema eneo hilo amepewa baada ya kuandika barua ya maombi kwa RAHCO na hatambui iwapo uzio huo umejengwa kimakosa kwa kuingilia njia ya treni wala iwapo kuna eneo linalomilikiwa na TBA ambalo uzio huo umeingilia.
Pia, aliongeza kuwa hatambui iwapo eneo hilo lina mgogoro na kuwepo kwa kesi mahakamani kwa kuwa yeye ni mpangaji tu na iwapo itafikia hatua ya kutakiwa kuvunja uzio huo,  hatokubali kuingia hasara na atahitaji kurejeshewa gharama zake za ujenzi kwa asilimia 50.
Mbali na eneo hilo la reli kuchukuliwa na mwekezaji huyo,  pia liko eneo la Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) ambalo limezua mgogoro mkubwa baina ya wakala huyo na RAHCO hadi kufikishana mahakamani kila mmoja akidai eneo hilo ni mali yake.
Akizungumza mbele ya Dk. Mwakyembe, msanifu majengo wa TBA, Pheres Tarimo, alisema eneo wanalogombania na RAHCO ni mali yao halali kutokana na mgawanyo wa mali za TRC uliofanyika miaka iliyopita na hati za umiliki na ramani zake wanazo ambazo walimkabidhi waziri huyo.
Pia, alisema mvutano huo ulisababisha RAHCO kukimbilia mahakamani kuwashitaki TBA kuwa ni wavamizi wa eneo hilo jambo ambalo liliwazuia kuendelea kuzungumzia suala hilo hadi kesi itakapomalizika.
Kutokana na maelezo hayo, Dk. Mwakyembe aliuagiza uongozi wa RAHCO kuiondoa kesi hiyo mahakamani mara moja kwa kuwa sio vyema kwa idara mbili za serikali kushitakiana na badala yake atawaita ofisini kwake ili kulizungumza suala hilo ambalo anaamini litamalizika.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru