Na Mwandishi Wetu
MAMBO yameendelea kuwa hovyo ndani ya CHADEMA, ambapo Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho, Zitto Kabwe anajiandaa kupeleka hoja ya kutaka kusafishwa dhidi ya tuhuma zilizotolewa na viongozi wenzake.
Lema aliweka katika mtandao, waraka ambao anazungumzia masuala ya posho na anashangaa watu wanaopinga posho wakati wanaishi katika maisha ya ufahari.
Waraka wa mbunge huyo, ulikuwa ukimlenga Zitto, ambaye naye alijibu kuwa kama kuna mbunge analilia posho hapaswi kufanya kazi ya ubunge na akafanye kazi nyingine.
Baada ya malumbano hayo, ulitolewa waraka na kada wa chama hicho, Henry Kileo, ambaye alieleza namna Zitto anavyonufaika kutokana na kukihujumu chama hicho.
Waraka huo ulioitwa wa siri ulieleza mambo mengi kuhusiana na Zitto ambaye alijibu kuwa hizo ni hekaya za abunuwasi na mwisho wake ni aibu.
Zitto alisema ameamua kuchukua wajibu huo ili kuokoa nchi kutoka kwenye makucha ya siasa za uongo, uzushi na uzandiki ili iwe fundisho kwa vifaranga na mama zao.
Taarifa zilizopatikana zilisema kikao hicho, kitakachofanyika mjini Dar es Salaam, mambo mbalimbali yatajadiliwa, ikiwemo uchaguzi wa chama na timuatimua ya viongozi inayofanywa na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.
Hali hiyo inatokana na baadhi ya viongozi kutimuliwa katika mikoa ya Arusha na Mara pamoja na kushindwa kuitishwa kwa uchaguzi kuanzia ngazi ya msingi, matawi, jimbo, wilaya, mkoa na taifa kama walivyopendekeza katika mpango mkakati wa chama hicho.
Mpango Mkakati wa Chama, ulifikiwa Januari, 2011, Bagamoyo, ambapo Kamati Kuu ilikiagiza chama kiwe kinaitisha uchaguzi mkuu wa chama kila baada ya miaka minne, ambapo hadi sasa uchaguzi bado haujafanyika licha ya kuamua mambo kadhaa.
Pia, waliamua uchaguzi wa chama ufanyike Septemba 2013 ili chama hicho kiweze kujipanga kwa uchaguzi mkuu wa urais, wabunge na madiwani.
Uhuru imepata taarifa katika kikao hicho kuwa, moja ya ajenda ni kutimuliwa kwa baadhi ya viongozi wa mikoa kunakofanywa na Mbowe.
Mwenyekiti huyo hadi sasa tayari ameshawatimua Wenyeviti wa mikoa ya Mara na Arusha, Samson Mwigamba (Arusha) na Machage Machage (Mara).
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru