NA MWANDISHI MAALUMU
RAIS Jakaya Kikwete amewasili mjini Colombo, Sri Lanka,
kuhudhuria Mkutano wa Wakuu wa Serikali za Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Madola (CHOGM).
Taarifa iliyotolewa jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Dar es Salaam, ilisema Rais Kikwete ambaye anaandamana na mkewe Mama Salma aliwasili jana mjini humo akitokea Dubai, Falme za Kiarabu, ambako aliwasili usiku wa jana akitokea nyumbani.

Aidha, viongozi hao, akiwemo Rais Kikwete watahudhuria hafla rasmi ya makaribisho itakayoandaliwa na Katibu Mkuu wa Jumuia ya Madola, Kamalesh Sharma katika Ukumbi wa Bandaranaike Memorial International Conference Hall (BMICH).
Jana, Rais Kikwete na Mama Salma, walitarajiwa kuhudhuria hafla ya chakula cha usiku kitakachoandaliwa na Prince Charles na mkewe, The Duchess of Corwall, kwenye hoteli ya Cinnamon Lakeside.
Jumuia ya Madola ni umoja wa nchi zilizokuwa chini ya ukoloni na himaya ya Uingereza na nchi nyingine ambazo zenyewe ziliomba na kukubaliwa kujiunga na Jumuia hiyo, zikiwemo Msumbiji na Rwanda.
Jumuia ya Madola ina jumla ya nchi wanachama 53, zikiwemo nchi 18 za Afrika ambalo ni bara lenye wanachama wengi zaidi katika jumuia hiyo, nchi nane za Asia, 13 za Marekani na Caribbean, tatu za Ulaya na 11 za Pacific.
Pia, jumuia hiyo ina mchanganyiko wa nchi kubwa na ndogo, nchi 32 kati ya hizo zilihesabiwa kama nchi ndogo kwa maana ya kuwa na idadi ya watu milioni 1.5 au chini ya hapo.
Sri Lanka ambayo mpaka mwaka 1972 ilijulikana kwa jina la Ceylon, inajulikama rasmi kama Jamhuri ya Kidemosia ya Kisoshalisti ya Sri Lanka. Ni nchi kisiwa kilichoko Kaskazini mwa Bahari ya India na Kusini mwa pwani ya nchi ya India. Ni nchi yenye mipaka ya maji na India na Maldives.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru