Na Chibura Makorongo, Shinyanga.
WATOTO wawili wa Kijiji cha Mangu, Kata ya Salawe wamejereuhiwa sehemu mbalimbali za miili yao baada ya kulipukiwa na chuma kinachodhaniwa kuwa ni bomu.
Habari zilisema chuma hicho kililipuka na kutoa moto ulioambatana na moshi mzito .
Watoto hao Fabian Philipo (9) na
Zawadi Konas, wanasoma darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Songambele ambapo chuma hicho kinadaiwa kilipelekwa na mtoto wa miaka mitano kikiwa ndani ya mfuko wa plastiki huku akikichezea na kuungana nao.
Hata hivyo, mkazi wa kijiji hicho James Fabian, alisema majira ya asubuhi saa mbili walishtuka kusikia mlipuko mkubwa uliofanya umati mkubwa wa watu kukimbia na kukusanyika katika nyumba iliyotokea sauti hiyo na kukuta watoto wameenea vumbi huku moto ukiwa umezima ila moshi mzito ukiendelea kufuka.
“Tulikuwa kijiweni majira ya asubuhi tukinywa kahawa, ghafla kikasikika kishindo kikubwa kilichoweka hofu kwa wananchi wa eneo hilo na wengine kukimbia hovyo, ila kuna baadhi tulijitoa mhanga kwenda kushuhudia na kukuta watoto wamelala chini wakiwa na vumbi huku moshi ukiendelea kufuka ndipo tuliwakimbiza zahanati,” alisema James.
Mama wa watoto hao aliyefahamika kwa jina la Pili Madata alisema watoto wake walikuwa nje wakicheza mwenyewe akiosha vyombo, mara akatokea mtoto wa jirani akiwa ameshika mfuko ambao ndani kulikuwa na kitu kama chuma ambacho walipokuwa wakikichezea ghafla kililipuka.
Alisema alikimbia ndani na kuwaacha watoto hao nje, muda mfupi aliwarudia na kuwakuta wakitokwa damu nyingi sehemu mbalimbali za miili yao.
Mganga Mfawidhi wa Mkoa, Frederick Mlekwa, alisema taarifa ya kupelekwa kwa watoto hao anayo ila bado hajafahamu hali zao zinaendeleaje ingawa walikuwa wanaendelea kupatiwa matibabu.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangalla, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuwa kitu kilicholipuka ni chuma kinachodhaniwa kuwa ni bomu.
Saturday, 2 November 2013
Watoto wajeruhiwa bomu wakilichezea
07:51
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru