Tuesday 5 November 2013

Sumaye awasha moto


Na Mwandishi Wetu
WAZIRI Mkuu mstaafu, Frederick Sumaye, ameibuka na kuwasha moto, huku akimtuhumu Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa kuwa amesema uongo kuhusu mradi wa maji katika Ziwa Victoria, kwamba ni jitihada zake binafsi.
Pia, amesema siku Chama Cha Mapinduzi (CCM), kikipitisha majina ya wagombea ambao ni wala rushwa na wauza dawa za kulevya kupeperusha bendera ya Chama, atakaa pembeni na ndio utakuwa mwisho wake kisiasa.

Amempongeza Rais Jakaya Kikwete kwa dhamira yake ya dhati ya kupambana na rushwa na ufisadi nchini, ikiwemo ndani ya CCM, ambako kuna baadhi ya wanachama na viongozi wamekuwa wakituhumiwa kushiriki.
Sumaye aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na masuala mbalimbali, na kuongeza wapo baadhi ya wanasiasa ambao wamekuwa wakizungumza uongo mkavu kwa lengo la kutafuta uongozi.
“Napongeza suala hili lipo na si ndani ya Chama pekee hadi nje. Rushwa ukiitazama unaweza ukasema ni suala dogo kati ya anayetoa na anayepokea, lakini ni tatizo kubwa kwa Watanzania. Hata hivyo, kuna mengi yanasemwa na wanasiasa, ambayo ni uongo mkavu, hivyo ni lazima tuyaweke sawa,” alisema Sumaye.
Alisema Septemba 16, mwaka huu, alishtushwa baada ya gazeti moja kumnukuu Lowassa alisema kuwa, kukamilika kwa mradi huo mkubwa uliopo mkoani Shinyanga ni juhudi zake binafsi zilizoungwa mkono na mawaziri wengine wawili, akiwemo Rais Kikwete, ambaye wakati huo alikuwa waziri.
“Lowassa anazungumza uongo mtupu. Hili suala lilianza zamani, kipindi ambacho hata hakuwa Waziri wa Maji. Alianza nalo Mheshimiwa Pius NgĂ­wandu, akaja Mussa Nkhangaa, ambao kwa kiasi kikubwa walimaliza kila kitu kuhusiana na mradi huo,” alisema.
Sumaye alisema kiutaratibu asingependa kulizungumzia suala hilo, hasa kutokana na kikao cha Baraza la Mawaziri kuwa siri na anayezungumza nje ya kikao ni kosa la jinai, lakini anashangazwa na Lowassa kuendelea kulizungumzia.
Alisema hiyo ni hatari, hasa kutokana na kujenga uhasama baina ya wananchi wa Shinyanga na serikali, lakini wananchi wanapaswa kujiuliza mbona alishindwa kupeleka maji Dodoma kipindi alipokuwa Waziri Mkuu.
“Natambua alisimamia mradi huo, lakini kwa maagizo ya serikali. Waziri huwezi kufanya jambo kubwa peke yako, na anaposema yeye amefanya hivyo, mbona alipokuwa Waziri Mkuu hakupeleka maji Dodoma?” alihoji Sumaye.
Taarifa kamili ya Sumaye aliyoitoa kwa vyombo vya habari jijini Dar es Salaam, jana inapatikana ukurasa wa 9 wa gazeti hili.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru